Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

SP MAGAYANE AWAONYA MADEREVA WANAOCHEZEA MFUMO WA VTS
Imewekwa: 04 Mar, 2025
SP MAGAYANE AWAONYA MADEREVA WANAOCHEZEA MFUMO WA VTS

 

SP Peter Magayane, Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Tabora amesema kuwa, endapo dereva atabainika kuchezea na kuharibu Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) wanapokuwa barabarani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Amebainisha hayo hivi karibuni kwenye ziara ya mafunzo ya siku mbili ya namna Mfumo wa VTS unavyo fanya kazi, alipotembelea Kituo cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari- VTS na Stendi Kuu ya Mabasi Magufuli Jijini Dar es salaam.

“Niwatahadharishe madereva ambao wanatabia ya kuchezea ving’amuzi vinavyofungwa kwenye mabasi kuwa waache mara moja tabia hiyo, na watambue kuwa wakija Mkoa wa Tabora wajue kwamba wanaenda sehemu ambapo kuna wataalamu ambao wameshapata elimu ya kutosha kuhusu Mfumo wa VTS na dereva yoyote atakayechezea Mfumo huu ajue kabisa atakutana na mkondo wa Sheria,” amesema SP Magayane.

Vilevile Bw. Emmanuel Aloyce, Msimamizi wa mifumo kutoka kampuni ya ICT PACK ambaye ametoa mafunzo ya Mfumo wa VTS anaelelezea umuhimu wa mfumo huo na kuwa ndio Mfumo mama wa Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaomuwezesha abiria kupata taarifa za mabasi yanayowasili kituoni.

“Kwenye ziara hii nimepata nafasi ya kuelezea namna Mfumo wa VTS unavyofanya kazi na namna ya kutambua viashiria vya mfumo uliochezewa kwa vitendo, mfumo huu wa VTS ndio Mfumo mama unaowezesha upatikanaji wa taarifa kwenye Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unapatikana kupitia anuwani ya www.pis.latra na kinga’muzi cha VTS kikichezewa hata mfumo wa PIS hautotuma taarifa kwa usahihi,” ameeleza Bw. Aloyce.

Wakati huohuo CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, amepongeza jitihada zinazofanywa na kikosi cha Usalama Barabarani kutoka Tabora na kuongeza kuwa kituo cha mabasi Nzega kinakwenda kuwa  kituo rasmi cha mabasi ili kutatua changamoto za usafiri wanazokutana nazo na kuahidi kurahisisha upatikanaji wa Mfumo  wa Taarifa kwa Abiria (PIS) katika stendi hiyo.

“Kituo cha Nzega kitakwenda kuwa kituo rasmi na mabasi yote yanayopita eneo hilo lazima yaingie pale na tutaweka runinga itakayoonesha Mfumo wa Taarifia kwa Abiria kama tulivyoweka stendi ya Magufuli Dar es Salaam na Stendi ya Mabasi Nanenane iliyopo Jijini Dododoma na abiria wataweza kupata taarifa za mabasi yanayowasili katika kituo hicho,” ameeleza CPA Suluo.

LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani wamejipanga kuhakikisha huduma za usafiri zinakuwa bora na salama hapa nchini.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo