
Mhe. Prof Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, ameshiriki katika Mkutano wa Nne wa Usafirishaji na Lojististiki kwa nchi zinazopitisha Shehena Zambia katika Ukanda wa SADC (Land-Linked Zambia 4th Conference). Mkutano huo unafanyika Lusaka, Zambia kwa siku mbili kuanzia tarehe 10 hadi 11 Aprili, 2025.
Mheshimiwa Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia alikuwa Mgeni Rasmi na Mkutano umehudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi za SADC, wawekezaji, wafadhili, wasafirishaji na wadau mbalimbali wa usafirishaji na lojistiki. Akifungua Mkutano huo, Mhe. Hichilema alisisitiza Umoja, ushirikiano wa kiuchumia, shughuli za kibiashara na uwekezaji katika Nchi za SADC bila kujali mipaka ya kijiografia.
Lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa usafirishaji na lojistiki katika nchi za SADC hususan shoroba mbalimbali ambazo zinatumiwa na nchi ya Zambia kupitisha shehena ya mizigo. Wadau hawa wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu na fursa zilizopo katika Nchi zao.
Katika Mkutano huo Mhe. Waziri Mbarawa atapata fursa ya kutoa maelezo na kuitangaza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu fursa mbalimbali za Uwekezaji katika sekta ya Usafiri na Usafirishaji kupitia shoroba zinazoiunganisha Tanzania na nchi za SADC. Uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali hususan katika Bandari, Reli ya SGR, TAZARA, Ujenzi wa Meli katika Maziwa Makuu na Uwepo wa Ndege ya Mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 54 ni maeneo muhimu Mheshimiwa Waziri atakayotolea taarifa katika mkutano huo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mbarawa ameambatana na viongozi mbalimbali akiwemo CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA.