Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

TRC KUSHINDANISHWA NA SEKTA BINAFSI KUTOA HUDUMA ZA USAFIRI WA RELI
Imewekwa: 17 Oct, 2023
TRC KUSHINDANISHWA NA SEKTA BINAFSI KUTOA HUDUMA ZA USAFIRI WA RELI

Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuharakisha kuandaa miongozo na leseni zitakazotolewa kwa wadau wa sekta binafsi watakaotumia miundombinu ya reli mara baada ya Kanuni za kuruhusu wawekezaji binafsi kwenye miundombinu hiyo kukamilika.

Dkt. Possi ameyasema hayo alipofungua mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu Rasimu za Kanuni za Watoa Huduma Binafsi za Usafiri wa Reli za Mwaka 2023, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam Oktoba 16, 2023.  

“LATRA muanze kuandaa miongozo na taratibu za kupata leseni kwa haraka na kwa uwazi bila kusahau eneo hili linaenda kuchochea ushindani kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC). Lengo ni kutimiza dhima ya Serikali ya kuongeza ufanisi katika usafiri wa reli na kuboresha utoaji wa huduma,” amesema Dkt. Possi.

Vilevile Dkt. Possi ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefungua milango kwa sekta binafsi katika kuchangia uchumi wa nchi kwa kuwa sekta hizo zina uwezo madhubuti wa kushiriki katika utoaji wa huduma ya usafirishaji kwa njia ya reli.

Aidha, amesema kuwa, ni wakati mwafaka kwenda na kasi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha uwekezaji na maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam, yanatuwezesha kuondosha mizigo kwa haraka kwa kupitia Reli.

Dkt. Possi ameongeza kuwa, kuwepo na ushindani wenye usawa kwa TRC na sekta binafsi itasaidia TRC kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma, “Nia yetu sisi mizigo isafiri, abiria wahudumiwe na Bandari yetu inufaike na kasi ya kukuza uchumi wetu uongezeke,” amesema Dkt. Possi.

Aidha Dkt. Possi ameitaka TRC kutafuta mshauri wa kitaalamu kwa haraka atakayeweza kuwapa maoni mazuri zaidi kuhusu kuwezesha watoa huduma binafsi kwenye miundombinu ya reli kulingana na mazingira ya nchi yetu.

Kwa upande wake CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, ameeleza kuwa LATRA kama mdhibiti  itasimamia vyema utoaji wa huduma za usafiri wa reli kwa sekta binafsi ili kuongeza ufanisi kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Uchukuzi, na amewakaribisha wadau kutoa maoni yao ili kuboresha Kanuni hizo.

“Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (Mb) ametoa maelekezo kwetu kama mdhibiti tuhakikishe tunatoa leseni kwa watu binafsi kutumia njia ya TRC kutoa huduma. Na tumefanya tathmini kwa mwaka 2019 hadi 2023 na kuona reli yetu inauwezo mkubwa wakusafirisha mizigo zaidi kutoka bandari yetu na kwenda sehemu mbalimbali hivyo niwakaribishe wadau wote watoe maoni ambayo yatasaidia kuleta kanuni zenye tija na zinazoendana na uhalisia” ameeleza CPA Suluo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za usafiri wa reli kutoka Wizara ya Uchukuzi Bw. Benjamin Mbimbi ameeleza kuwa, Serikali itaweka utaratibu maalum ambao utawezesha watoa huduma binafsi kutekeleza majukumu yao na Serikali kupata mapato yake.

“Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika kutoa huduma kwa kununua mabehewa na vichwa vya treni na kupitia Kanuni hizi kutakuwa na utaratibu maalum wa kulipia ada ya kutumia njia ya treni ya TRC, huku jukumu la kumiliki na kuboresha miundombinu litabaki kuwa la Serikali, hii pia itasaidia katika kuongeza kasi ya uchumi katika sekta ya reli nchini” ameeleza Bw. Mbimbi.

Ili kuboresha Kanuni za usafirishaji kwa njia ya reli wadau wamepewa siku 14 kuwasilisha maoni yao kwakuwa ni muhimu katika kuboresha utoaji huduma wa Usafiri wa reli kwa wananchi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo