
Na Mambwana Jumbe
Umeshawahi kusafiri na basi kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine? Katika Safari yako umeshawahi kusikia muito wa kengele ukipiga katikati ya safari? Kengele hiyo uliichukuliaje? Ulielewa maana yake na kuchukua hatua au uliiacha na kuona kuwa ni kelele za kawaida? Kengele unayoisikia ukiwa safarini kwenye basi ni kiashiria ya kwamba gari hilo limefikia au limezidisha mwendo ulioidhinishwa na Serikali yaani linaendeshwa kwa mwendokasi wa kilometa 80 kwa saa au zaidi na hivyo inahatarisha maisha yako na wengine waliopo ndani ya basi hilo.
Suala la ajali barabarani limekuwa likigharimu maisha ya Watanzania wengi hapa nchini. Wapo wanaopoteza maisha, wapo wanaopoteza viungo nakusababishiwa ulemavu wa kudumu na wapo wanaoachwa yatima kwa kupoteza wapendwa wao kwenye ajali. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakisikitishwa sana na hali hii kwa kuwa nguvu kazi ya Taifa imekuwa ikipotea na imefanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba changamoto ya ajali barabarani inapungua au kuondoka kabisa.