Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa jumla ya vibali 169 vya safari kwa mabasi yanayosafiri kuanzia Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali Tanzania Bara kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za usafiri kwa abiria kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa Desemba 15, 2025 na Bi. Rukia Kibwana, Afisa Mfawidhi LATRA Kituo Kikuu cha Mabasi Magufuli Dar es Salaam ambapo amesema vibali hivyo vya muda hutolewa mwisho wa mwaka kutokana na ongezeko la abiria wanaosafiri kwenda mikoani.
“Kuanzia Novemba 30, 2025 hadi kufikia leo jumla ya vibali 169 vimetolewa katika Mikoa yote Tanzania Bara kwa mabasi yanayosafiri mikoa mbalimbali nchini, vibali hivyo vimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongano wa abiria kituoni hapa kwa nyakati tofauti hasa nyakati za asubuhi na jioni ambapo abiria ni wengi zaidi,” amesema Bi. Kibwana.
Bi. Kibwana ameeleza kuwa awali Mamlaka ilianza kwa kutoa vibali 72 kwa mikoa ya Iringa, Dodoma, Morogoro na Tanga ambapo uhitaji wa safari za abiria ulionekana kuwa ni mkubwa.
Pia ameeleza vigezo vilivyozingatiwa kutoa vibali hivyo ni, mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria 40 na kuendelea au iwe na leseni ya Mabasi Maalum ya Kukodi (Special Hire), basi liwe limeunganishwa kwenye Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), dereva awe na Kitufe cha Utambuzi (i- Button) kilichosajiliwa na LATRA na basi liwe limeunganishwa kwenye Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi.
Aidha Bi. Kibwana amesema, Mamlaka imewataka wananchi kuendelea kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka akifafanua kuwa, LATRA inafahamu idadi kubwa ya uhitaji kwa abiria hivyo inaendelea kusimamia na kuratibu huduma za usafiri kwa kuongeza vibali vya usafiri.
Mamlaka imekuwa na utaratibu unaofanyika kila mwaka kutoa vibali vya muda inapofika kipindi cha mwisho wa mwaka kuelekea sherehe za Krismas na Mwaka mpya kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa huduma za usafiri kwa abiria unaimarika.

