Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WADAU WA KAMATI YA URATIBU USALAMA WA USAFIRI ARDHINI WAKUTANA
Imewekwa: 10 Jan, 2023
WADAU WA KAMATI YA URATIBU USALAMA WA USAFIRI ARDHINI WAKUTANA

Na Mambwana Jumbe

Kamati ya Uratibu Usalama wa Usafiri Ardhini imeendesha kikao kazi cha pamoja na wadau wa Sekta ya Usafiri Ardhini kujadili na kutathmini hali ya usafiri na usafirishaji kwa kipindi cha Desemba 2022 hadi Januari mwanzoni, 2023.  

Akielezea utekelezaji wa mikakati iliyowekwa na Mamlaka kudhibiti changamoto za usafiri kwa mwezi Desemba, 2022, Meneja wa Usalama na Mazingira kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Bw. Geoffrey Silanda, ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao kazi hicho alisema Mamlaka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani walishirikiana kwa kufanya ukaguzi wa pamoja wa mabasi ya masafa marefu, ukaguzi wa barabara kuu pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva.

“Tuliongeza mabasi ya kwenda mikoani na tulitoa mapema tangazo la kuomba Leseni za Muda mfupi ambapo wasafirishaji walijitokeza kwa wingi na kupata leseni hizo na jumla ya leseni za muda mfupi zilizotolewa ni 236 kati ya hizo 77 zimetolewa Dar es salaam na 159 mikoani jambo ambalo lilisaidia sana kudhibiti suala la upungufu wa usafiri kwa abiria.” Bw. Silanda alieleza.

Aliongeza kuwa Desemba 17, 2022, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (MB) alitoa maelekezo ya Serikali kwa Mamlaka ya kufanya mabadiliko madogo kwenye ratiba za baadhi ya mabasi ili yaanze safari kuanzia saa 11:00 alfajiri, “Sisi kama wadhibiti tuliwahabarisha wasafirishaji na agizo hili likaanza kutekelezwa mara moja na kwa kweli ilisaidia sana kukabili adha ya usafiri kwa kipindi hicho.”

Katika kudhibiti suala la abiria kuzidishiwa nauli, Bw. Silanda alisema kuwa matumizi ya tiketi za kielektroni yalisaidia kuondoa kero hiyo kwa kuwa abiria wengi walikata tiketi hizo kwa njia ya mtandao.

Naye Bw. Frank Shangali, kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) Kanda ya Mashariki ameipongeza Mamlaka kwa hatua madhubuti ilizochukua ikiwemo kuondoa adha ya usafiri kipindi cha mwisho wa mwaka 2022 na Januari 2023 na ametoa wito kwa Mamlaka na wadau wengine kujipanga zaidi kwa miaka inayokuja ili kuondoa kabisa changamoto ambazo hujitokeza kipindi cha mwisho wa mwaka.

Naye Bi. Fatuma Kulita Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala kutoka Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao pindi wanapotaka kusafiri ili kuepukana na kadhia za usafiri na hata kama ikitokea ajali, ni rahisi kupata stahiki.  

Kikao kazi hicho kimefanyika Januari 10, 2023 katika ofisi za LATRA Dar es Salaam na kimehudhuriwa na washiriki kutoka LATRA, Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA Tanzania), Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

 

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo