Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WADAU WA USAFIRISHAJI WAASWA KUTII SHERIA
Imewekwa: 27 Nov, 2025
WADAU WA USAFIRISHAJI WAASWA KUTII SHERIA

Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewasihi wadau wa sekta ya usafiri ardhini nchini wakiwemo watoa huduma na watumiaji wa huduma za usafiri kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za usafiri ardhini zilizopo ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.

Dkt. Nchemba amebainisha hayo alipofungua rasmi Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025, Novemba 26, 2025 Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.

 “Nitoe rai kwa wadau wote kutekeleza Sheria za usafirishaji nchini pamoja na kuitunza miundombinu iliyotengenezwa na kuboreshwa na Serikali kwa gharama kubwa. Miundombinu hii inawawezesha wananchi kuinua uchumi wao kupitia biashara ya usafirishaji abiria na mizigo,” ameeleza Mhe. Nchemba.

Wakati huohuo, Dkt. Nchemba amezitaka taasisi zinazohusika na kusimamia Sheria za usafirishaji zilizowekwa kwa ajili ya wananchi kuhakikisha Sheria hizo zinasimamiwa vizuri na kutekelezwa bila kubagua.

Kwa upande wake CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa LATRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo, na itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani katika kutekeleza majukumu yake, hususan kupambana na ajali za barabarani.

Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini imeipa LATRA jukumu la kudhibiti sekta ndogo tatu ambazo ni sekta ya usafiri wa barabara, usafiri wa reli na usafiri wa waya.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo