Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WAHUDUMU 67 WA MABASI YA MASAFA MAREFU NA MIJINI KANDA YA KASKAZINI WAHITIMU MAFUNZO
Imewekwa: 09 Feb, 2024
WAHUDUMU 67 WA MABASI YA MASAFA MAREFU NA MIJINI KANDA YA KASKAZINI WAHITIMU MAFUNZO

Wahudumu 67 wa mabasi ya masafa marefu na mijini Kanda ya Kaskazini Tanzania Bara wamehitimu mafunzo yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) pamoja na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuanzia Februari 5-9, 2024 katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Wahudumu hao wamejifunza masuala mbalimbali ikiwemo Sheria, Kanuni na Taratibu za LATRA, Huduma bora kwa usalama wa abiria na mali, Namna ya kukabiliana na malalamiko ya wateja, Huduma ya kwanza kwa mteja, Utunzaji wa mizigo pamoja na kutambua bidhaa hatarishi, Mfumo wa Tiketi Mtandao, Muitikio wa dharura, Uhusiano na mawasiliano, Unadhifu wa mtoa huduma pamoja na  Utunzaji wa mazingira.

Bw. Hadney Chikukuro, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Uchumi na Rasilimali alimwakilisha Mhe. John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwenye hafla ya ufungaji wa mafunzo kwa wahudumu wa mabasi ya masafa marefu na mijini Kanda ya Kaskazini, Tanzania Bara yaliyofanyika katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Februari 9, 2024.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mhe. Mongella, Bw. Chikukuro amewaasa wahudumu hao kutumia maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na ufanisi ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wateja wao.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wateja wenu hasa katika namna mnavyowahudumia, ni matumaini yangu kwamba baada ya mafunzo haya mnaenda kubadili utendaji kazi wenu. Pia nawasihi kuyazingatia yote mliyofundishwa na muende kuyatekeleza kwa vitendo ili kuwa na usafiri ardhini ulio na tija,” ameeleza Bw. Chikukuro.

Vilevile, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya usafiri ardhini ikiwa ni pamoja na kuiheshimisha kada ya wahudumu na kuifanya kuwa yenye tija kwa kuwa ni kazi kama kazi nyingine.

Pia, Bw. Chikukuro ametoa wito kwa uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi  kwa weledi mkubwa ili kukifanya Chuo hicho kuwa mahali sahihi pa kupatia mafunzo stahiki na ametoa rai kwa Chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara ili kuhakikisha wahudumu wanaendelea kutoa huduma zinazokidhi vigezo kwa abiria wao.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewapongeza wahudumu waliohitimu mafunzo na amewaeleza kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa mujibu wa Sheria ambapo kwa mujibu wa Kifungu Na 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, Mamlaka ina jukumu la Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara.

“Tunawapongeza kwa kuwa ninyi ni wahudumu wa kwanza kupata mafunzo haya na baada ya hapa, tutawapatia vitambulisho vitakavyoonesha kuwa mnatambuliwa na LATRA. Ninawasihi mkaoneshe utofauti mnapotekeleza majukumu yenu na sisi tutawafuatilia ili kuona utekelezaji wa yale mliyofundishwa,” ameeleza CPA Suluo.

Kwa upande wake Dkt Zainabu Mshana, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ameishukuru LATRA kwa ushirikiano na ameahidi kuwa mafunzo hayo yataendelea kutolewa katika Kanda nyingine ili kuwafikia wahudumu wengi nchini.

Vilevile amewasihi wahudumu hao kuwa mabalozi wazuri kwa wahudumu wengine ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria kwenye mafunzo kwa kuwaelekeza masuala muhimu ya kuzingatia pindi wanapotekeleza majukumu yao ili kuifanya sekta ya usafiri ardhini kuwa bora.

Naye Dkt. Cairo Mwaitote amesema mafunzo hayo yataleta chachu katika maendeleo ya sekta ya usafiri ardhini kwa kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo, Bi. Fatma Ally amewashukuru wakufunzi kwa kuwafundisha kwa umahiri na wameahidi kuyatekeleza waliyofundishwa kwa vitendo.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo