Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WAMILIKI WA KAMPUNI YA MABASI YA SAULI NA NEWFORCE WATAKIWA KUJIELEZA
Imewekwa: 03 Apr, 2024
WAMILIKI WA KAMPUNI YA MABASI YA SAULI NA NEWFORCE WATAKIWA KUJIELEZA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri ardhini (LATRA) imewataka wamiliki wa mabasi ya Sauli na New Force kutoa maelezo kwa maandishi kabla ya kuchukua hatua za kiudhibiti juu yao kufuatia ajali iliyohusisha basi lenye namba ya usajili T175DZU ya kampuni ya New Force na basi lenye usajili T668 DTF Scania mali ya Mwalabhila Sauli Machi 28, 2024 Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani.

Amesema hayo Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara wakati wa kikao kilichohusisha LATRA, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na wawakilishi kutoka mabasi ya Sauli na Newforce Aprili 2, 2024 katika ukumbi wa mikutano ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

“Tumebaini kuwa ajali imetokana na uzembe wa madereva na kuwa hakuna usimamizi mzuri wa kampuni hizi katika kutekeleza masharti ya leseni ya usafirishaji. Hivyo kufuatia kikao hiki kampuni hizi ziwasilishe maelezo kwa maandishi kabla ya kuchukua hatua za kiudhibiti dhidi yao,” amesema Bw. Kahatano.

Vilevile amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) Mamlaka imebaini kuwa madereva waliokuwa wakiendesha mabasi hayo kwa siku hiyo hawakutumia kitufe cha utambulisho (I-Button) kabla ya kuanza safari jambo ambalo ni kinyume na masharti ya leseni zao.

Naye ACP. Michael Deleli, Mkuu wa dawati la elimu ya Usalama Barabrani Tanzania amewakumbusha wasafirishaji kutekeleza majukumu yao na utendaji katika kuwasimamia madereva.

“Sisi kama Jeshi la Polisi tunawakumbusha wamiliki wa kampuni za usafirishaji kutekeleza vyema majukumu yenu kwa kuwafuatilia madereva kwa ukaribu pamoja na kutafuta madereva wanaojitambua wawapo barabarani,” amesema ACP Deleli.

Ameongeza kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakikutwa na vimiminika vyenye ulevi jambo ambalo ni kinyume na Sheria na amewasihi kuacha uzembe barabarani ili kunusuru maisha ya Watanzania na mali zao.

Kwa upande wao wawakilishi kutoka mabasi ya Newforce na Sauli wamekiri kuwa ajali iliyotokea imesababishwa na uzembe wa madereva wao na wamejipanga kuendelea kutoa elimu kwa madereva hao kwa kushirikiana  na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha Usalama wa abiria na mali zao unakuwepo.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo