Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WANANCHI WAKOSHWA NA LATRA SABASABA
Imewekwa: 11 Jul, 2024
WANANCHI WAKOSHWA NA LATRA SABASABA

Wadau mbalimbali wa usafiri nchini wametembelea jengo la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kujifunza kazi na majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na LATRA kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (sabasaba) katika viwanja vya Julius Nyerere yanayoendelea kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2024.

Akizungumza baada ya kutembelea Jengo la LATRA na kupatiwa elimu kuhusu  Mamlaka inavyotekeleza majukumu yake, Bw. Damian Patrick, Mdau wa Usafiri Ardhini na amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa na LATRA na jinsi huduma hizo zinavyokuwa msaada kwa wananchi,

“Kwa kweli, nimeridhishwa na LATRA kwa huduma nzuri wanayotoa katika maonesho haya kwani nimepokelewa vizuri na kujifunza mengi hususan Mifumo yao ya kidigitali ya kufuatilia mwenendo wa mabasi. Pia, huduma za kutoa leseni za usafirishaji kwani wameturahisishia sisi wadau kupata leseni zetu kwa urahisi kupitia mfumo wa maombi ya leseni na kizuri zaidi kwa sasa tunachapa wenyewe leseni na hatuna haja ya kwenda kwenye ofisi zao kufuata leseni,” amesema Bw. Patrick.

Kwa upande wake Bi. Neema Mkwera, mdau wa usafiri ameeleza kuwa, “nimejifunza mengi kutoka LATRA na kufahamu kuwa wapo kwa ajili ya kusimamia usalama barabarani kwani wanaweza kudhibiti mwendo wa mabasi wakati wowote na kuhakikisha usalama wa abiria tunapokuwa safarini pamoja na kututoa wasiwasi tunapokuwa safarini.”

Naye Bw. Chilo Raphael, mhudumu wa mabasi ya mijini (Daladala) ameonesha kufurahia huduma za LATRA alizozipata katika Jengo hilo ikiwa ni pamoja na kuwasilisha changamoto za usafiri katika jijini Dar es Salaam.

“Nafurahishwa na usimamizi mzuri wa LATRA katika sekta ya usafirishaji, naiomba Mamlaka kwa niaba ya makondakta wenzangu kutusaidia kusafirisha abiria kwa urahisi bila changamoto zozote hasa kutuongezea vituo vya kuwashusha abiria kwani hili swala limekuwa kilio chetu kikubwa,” ameeleza Bw. Raphael.

Naye Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA amewashukuru wadau mbalimbali waliotembelea jengo la LATRA kwa kujifunza mengi kuhusiana na LATRA.

“Nawashukuru wadau na viongozi mbalimbali waliotutembelea hapa sabasaba kwa lengo la kufahamu kazi na majukumu tunayoyatekeleza kwani wameshuhudia mengi kuhusu Mamlaka na wametushauri maeneo ya kuboresha ili kwa pamoja tuwe na sekta ya usafiri ardhini yenye tija kwa wananchi, wasafirishaji pamoja na Serikali kwa jumla.”

Katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (sabasaba), wananchi wanapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo usafiri ardhini ikiwa ni pamoja na matumizi ya Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na mfumo mpya wa Taarifa kwa Abiria (PIS – Passenger Information System).

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo