Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WASAFIRISHAJI KIGOMA WAASWA KUZINGATIA MASHARTI YA LESENI.
Imewekwa: 09 Sep, 2023
WASAFIRISHAJI KIGOMA WAASWA KUZINGATIA MASHARTI YA LESENI.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo ametoa wito kwa wasafirishaji Mkoani Kigoma kufuata misingi ya Sheria, Kanuni na taratibu za utoaji huduma hiyo ili kuweka usawa katika utoaji huduma na kuepusha malumbano yasiyo na tija katika Taifa.

CPA Suluo ameyasema hayo hivi karibuni katika mkutano na wadau ulioandaliwa na LATRA katika ukumbi wa Kigoma Social Hall ili kutoa elimu ya majukumu ya LATRA kwa mujibu wa Sheria na kupokea maoni ya wadau hao kuhusu changamoto zinazowakabili katika shughuli za usafiri na usafirishaji katika mkoa huo.

Aidha, CPA SUluo amesema kila msafirishaji anayedhibitiwa na Mamlaka anatakiwa kufuata masharti ya leseni hizo na si kufanya kadiri wanavyojiskia, “Baada ya kusikia yote tuliyoyajadili hapa nitoe wito sasa kwa wasafirishaji wote tufuate Sheria ambazo zinatuongoza katika utoaji wa huduma, magari ya kukodi ni ya kukodi na yafanye shughuli hiyo, daladala isafirishe kama daladala na hata kwa vyombo vingine kwa sababu kila mtu anapewa leseni ya usafirishaji basi kila mtu afuate masharti ya leseni aliyopewa.”

Aidha CPA Suluo amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mazingira mazuri ya utendaji kazi anayoyaweka na kuwapongeza wadau kwa kuendelea kutoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo kwa niaba ya Serikali.

“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA, Menejimenti na Wafanyakazi wa LATRA tunapenda kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mazingira wezeshi ya kufanyia kazi anayotuwekea, kiukweli naona kazi yangu inakuwa nyepesi, pia niwapongeza kwa jumla kwa kuendelea kutoa huduma bila kuchoka kwani mmekabidhiwa dhamana hii kwa niaba ya serikali,” ameongeza CPA Suluo.

Kwa upande wake Bw. Jahansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara amewasisitiza wasafirishaji kuwaza na kujali maslahi ya abiria ambao ndio wateja wao wakati wanapofanya biashara badala ya kuwaza faida itokanayo na biashara hiyo.

“Wote tumeshuhudia katika majadiliano yetu hakuna sehemu hata moja ambayo tumemtaja abiria, kila mmoja ametoa hoja kuvuta upande wake lakini hakuna hoja ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya kumsaidia abiria, hivyo niwaombe mzingatie maslahi ya abiria mnapoendesha shughuli zenu na mtambue kuwa abiria mnaowahudumia ni wananchi wa hali ya chini,” amesema Bw. Kahatano.

Naye Bw. Rashid Mechos, mdau wa usafiri Mkoanini Kigoma ameipongeza LATRA kwa kuwafikia wadau moja kwa moja na kuwapa elimu pamoja na kusikiliza kero zinazowakabili wadau hao huku akiamini mkutano huu unakwenda kuleta matunda chanya.

“Ni mara yangu ya kwanza kushuhudia Mkurugenzi Mkuu anafika hadi kwa wadau moja kwa moja, niwapongeze sana kwa busara na hekima mliyoitumia, naamini kuwa hata pande ambazo zilikuwa zikikinzana elimu wameipata na watakwenda kubadilika,” amesema Bw. Mechos.

LATRA imekuwa na utaratibu wa kukutana na wadau wa usafiri ardhini kila mara ili kutoa elimu na wakati mwingine kuwashirikisha pale Mamlaka inataka kufanya uamuzi wa jambo lenye maslahi kwa umma, hivyo ushiriki wa wadau kikamilifu ni muhimu ili kuhakikisha mawazo yao yanajumuishwa kwenye uamuzi.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo