Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WASAFIRISHAJI WAASWA KUFUATA SHERIA ZA KIMATAIFA
Imewekwa: 15 Jan, 2023
WASAFIRISHAJI WAASWA KUFUATA SHERIA ZA KIMATAIFA

Na Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewakumbusha madereva wa magari ya mizigo kufuata Sheria ya Usafirishaji ya Kimataifa.

Akizungumza wakati wa kikao na wadau wa usafirishaji wa magari ya mizigo jijini Dar es Salaam Januari 13, 2023, Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amewataka madereva wanaokiuka sheria kuchukua tahadhari kwani inaweza kusababisha hasara kwa wamiliki.

“Sheria inazuia magari yanayotoka nje ya nchi kuja Tanzania halafu yakasafirisha mizigo ndani ya Tanzania pia tunapokwenda nchi za wenzetu tukifika kule hatupaswi sisi tena kuchukua abiria au mizigo kwenda sehemu ya ndani au nchi jirani, wenzetu Malawi wanaweka sheria kwamba sasahivi ukienda Malawi ukafanya biashara bila kuwa na leseni ya kule wanakutaifishia magari “, alisema CPA Suluo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara Bw. Johansen Kahatano aliwaambia wadau kuwa Mamlaka imeanza kuwasajili madereva ili ikitokea dereva amevunja Sheria, mmiliki asihusike moja kwa moja.

Naye Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani SACP Ramadhani Ng’anzi ameipongeza LATRA kwa kuitisha kikao hicho na alisema Jeshi la Polisi limeandaa mikakati madhubuti ya kutenganisha dereva na mmiliki kutokana na makosa wanayoyafanya madereva.

“Na sisi tutaimarisha mifumo yetu ya kubaini na kujua makosa ya Usalama Barabarani ili mifumo hiyo iweze kumtambua dereva peke yake “, alifafanua SACP Ng’anzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TAMSTOA) Bw. Chuki Shabani alisema, “Nina imani yale tuliyoongea hapa yamechukuliwa kwa uzito na LATRA na Jeshi la Polisi na pia yatafanyiwa kazi”.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo