Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WASAFIRISHAJI WAASWA KUZINGATIA KANUNI ZA LESENI ZA USAFIRISHAJI MAGARI YA ABIRIA ZA MWAKA 2020
Imewekwa: 12 Feb, 2023
WASAFIRISHAJI WAASWA KUZINGATIA KANUNI ZA LESENI ZA USAFIRISHAJI MAGARI YA ABIRIA ZA MWAKA 2020

Na Mambwana Jumbe

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa wito kwa wasafirishaji kuzingatia Kanuni za Leseni za Usafirishaji Magari ya Abiria za mwaka 2020 ikiwemo ya kuwapatia abiria tiketi za kielektroni.

 Hayo yameelezwa na Meneja Mradi Tiketi Mtandao CPA Tadei Mwita kwenye semina na wamiliki wa mabasi iliyofanyika Februari 12, 2023 jijini Arusha

CPA Mwita amesema Kanuni ya 22(j) inamtaka mwenye leseni ya kusafirisha abiria kutoa tiketi kwa kutumia mfumo wa tiketi wa Kielektroni ulioidhinishwa na LATRA na Kanuni ya 23(b) na 24(d) inamtaka mwenye leseni ya kusafirisha abiria ahakikishe tiketi ya kielektroni inatolewa kwa kila abiria.

“Kwa mujibu wa hizi kanuni, msafirishaji atapaswa kuhakikisha mda wote anapofanya kazi ya kusafirisha abiria anatoa tiketi kwa kutumia mfumo huu na kwa kila abiria ambae anapanda kwenye basi apewe tiketi ambayo ni ya kieletroni,” amefafanua CPA Mwita

Vilevile amewaasa abiria kukata tiketi kwa kupitia simu janja ili kuepuka usumbufu wa wapiga debe kwenye vituo vya mabasi, “Tuwaombe abiria wasihangaike kwenda kwenye vituo vya mabasi wakate tiketi popote walipo bila kulazimika kwenda kwenye kituo cha mabasi lakini kwa upande wa usafirishaji wahakikishe mabasi yanapatikana kwenye mifumo ili abiria aweze kujihudumia pale alipo.”

Aidha, CPA Mwita amewasihi wamiliki hao kuendelea kusoma na kuzifuata Kanuni za Usafirishaji Magari ya Abiria za mwaka 2020 zinazopatikana kwenye tovuti ya Mamlaka kupitia anwani www.latra.go.tz

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Bw. Salum Pazzy, amesema LATRA imekutana na wamiliki hao ili kuwapatia elimu ya matumizi ya tiketi mtandao na kusikiliza changamoto zao hasa mkanganyiko wa matumizi wanayofanya na kushindwa kutambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa kufanya makadirio ya kodi

 “Wameeleza changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ya upotevu wa mapato ambapo kwa pamoja tumeona suluhisho mojawapo ni kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao,” amesema Bw. Pazzy

Kwa upande wa Meneja wa EFD Bw. Mabula Sambayuka, amesema ni muhimu wasafirishaji kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao ili wanapotoa tiketi ziwe na vigezo vyote kwa kuondoa changamoto wanazokutana nazo hasa pale wanapotumia tiketi zisizo za kielektroni na kuonekana wanakwepa kodi.

Naye Bw. Haruna Kakiva alishiriki semina hiyo ambaye amesema ameridhishwa na ushirikishwaji kwa kuwa unaimarisha uhusiano kati yao wamiliki wa mabasi na Mamlaka husika ambazo ni LATRA na TRA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo