Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WASAFIRISHAJI WATAKIWA KUUNGANISHA MFUMO WA TIKETI MTANDAO NA MFUMO WA TRA
Imewekwa: 26 Jan, 2023
WASAFIRISHAJI WATAKIWA KUUNGANISHA MFUMO WA TIKETI MTANDAO NA MFUMO WA TRA

Na Mambwana Jumbe

Wadau wa usafirishaji wametakiwa kuunganisha Mfumo wa Tiketi Mtandao na Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuwezesha taarifa za ukataji wa tiketi kufika moja kwa moja kwenye Mamlaka hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Bw. Johansen Kahatano kwenye kikao cha pamoja na wadau wa usafirishaji, kilichofanyika katika ofisi za LATRA Dar es salaam Januari 25, 2023 ambacho kilihudhuriwa na wadau kutoka Chama cha Wamiliki wa MabasiTanzania (TABOA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).

Bw. Kahatano amesema, “Wapo watoa huduma wachache waliounganisha mfumo wao na TRA lakini wengine bado hawajafanya hivyo, na tumepeana muda mpaka kufikia Januari 31, 2023 wadau wote wawe wameshaunganisha mifumo yao kwenye mfumo mama wa TRA ili taarifa zote za tiketi zinazokatwa zionekane TRA kwa lengo la kufuatilia mapato yanayotokana na huduma ya usafirishaji.”

Kwa upande wake Katibu Mkuu Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) Bw. Joseph Priscus, amesema wao kama wasafirishaji wametoa maoni yao kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwamba baadhi ya Sheria zake zinazosimamia upande wa mabasi ziendane na mazingira ya usafirishaji lakini pia Sheria ziweze kutenganisha makosa kati ya mmiliki wa chombo cha usafiri, dereva na kondakta.

“Tunaomba TRA watengeneze Sheria ambayo kila mtu awajibishwe kwa kosa lake kama vile kosa la dereva awajibike dereva, kosa la kondakta awajibike kondakta na kosa la mmiliki wa gari awajibike mmiliki. Lakini tunashukuru tumesikilizwa kuna mambo yanaenda kufanyiwa kazi na TRA,”ameeleza Bw. Priscus.

Naye Bw. Gerald Katawanya, Meneja Mradi kutoka Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) ameshukuru kwa kushirikishwa kwenye kikao hicho na amesisitiza suala la utoaji wa elimu kuhusu Tiketi Mtandao kwa watumiaji lakini pia kwa baadhi ya wasafirishaji ambao bado hawajaanza kutoa huduma kupitia Tiketi Mtandao ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa katika mfumo huo.

“Mfumo wa Tiketi Mtandao una umuhimu na faida kubwa ikiwemo kuokoa muda ambao abiria anatumia wakati wa kwenda kukata tiketi katika ofisi za mabasi, kuepuka changamoto za wapiga debe lakini pia husaidia abiria kupata stahiki zake endapo itatokea ajali au madhara yoyote kwa kupewa fidia na bima,” amefafanua Bw. Katawanya.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo