Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewatia mbaroni mawakala watano wasio rasmi kwa kosa la kukiuka masharti ya leseni ikiwemo kutoza nauli kuliko kiwango kilichopangwa na Mamlaka pamoja na kutotoa tiketi za kielektroni.
Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 6, 2025 Kituo Kikuu cha Mabasi Magufuli Dar es Salaam baada ya ukaguzi wa kushtukiza, CPA Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, Mamlaka imefikia hatua hiyo baada ya kuwabaini mawakala ambao hawajasajiliwa na LATRA maarufu kama masarange wanaowadanganya abiria wa mabasi ya masafa marefu kwa kuwauzia tiketi za makaratasi zisizo halali.
“Timu ya ukaguzi imebaini watu wenye tiketi mkononi zisizo halali kuanzia 20 hadi 30 zenye nauli kubwa na abiria wamekuwa wakiuziwa tiketi za safari za mabasi kwa bei ya juu na wakifika kwenye mabasi wanakuta nauli halisi ni ndogo au basi walilokatiwa tiketi halipo kabisa, watuhumiwa hao tayari wapo chini ya ulinzi na taratibu za kuwafikisha katika vyombo vya Sheria unaendelea,” amesema CPA Dkt. Suluo.
Vilevile amesema kuwa, baadhi ya kampuni za mabasi zilizohusika kuwatoza abiria nauli zaidi ya iliyoelekezwa na LATRA ni kampuni ya Haji’s na Takbiir zinazofanya safari za Dar es Salaam - Lushoto ambapo Mamlaka imewaelekeza kurejesha nauli za abiria ambao wamewazidishia na huku wakitozwa faini kama sehemu ya adhabu ya makosa yao.
Kwa upande wake Bruno Samweli, abiria kutoka Mbagala Rangi Tatu akisafiri kuelekea Kahama amesema, kumekuwa na changamoto kutokana na uwepo wa walanguzi wa tiketi ambao hununua tiketi mtandaoni kisha kuuza kwa bei isiyoelekezwa na Mamlaka na amewashauri wanaokiuka taratibu hizo kufuata Kanuni na Sheria za leseni zao ili kuepusha kujiingiza kwenye makosa yasiyo ya lazima .
Naye Sophia Kanengene, Msafiri kutoka Mbezi Luis kuelekea Geita – Katoro abiria aliyezidishiwa nauli ameishukuru Mamlaka kwa hatua waliyoichukua ya kuwakamata watuhumiwa hao na kuwapambania abiria waliozidishiwa nauli kurejeshewa nauli zao kwani wamekuwa wakitoza fedha nyingi bila wao kujua.
Kwa upande wao mawakala waliotiwa mbaroni wamekiri kutoza nauli isiyoidhinishwa na LATRA na kuwa wamewarejeshea abiria nauli zao baada ya kuwajibishwa na LATRA na wamewasihi mawakala wenzao kujitokeza kusajiliwa rasmi na LATRA na kuachana na vitendo hivyo.
Mamlaka inaendelea kufanya kaguzi mbalimbali mikoa yote Tanzania Bara kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri ardhini zilizokuwa bora na salama.

