Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

WATOA HUDUMA ZA MIFUMO YA TIKETI MTANDAO WATAKIWA KUJISAJILI NA MFUMO WA TRA EFDMS KABLA YA MEI 31, 2024
Imewekwa: 01 May, 2024
WATOA HUDUMA ZA MIFUMO YA TIKETI MTANDAO WATAKIWA KUJISAJILI NA MFUMO WA TRA EFDMS KABLA YA MEI 31, 2024

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA)  amesema Mei 31, 2024 ndio muda wa mwisho kwa watoa huduma za Mfumo wa Tiketi Mtandao kuunganisha mifumo yao na Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Risiti za Kielektroni (EFDMS) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mifumo ya Tiketi Mtandao wa Mabasi ambayo haitaunganishwa na mfumo wa TRA EFDMS ili kukidhi hitaji la kisheria la matumizi ya EFD kwa wafanyabiashara ya usafirishaji abiria haitaruhusiwa kutumika kuanzia tarehe 15 Juni, 2024.

CPA Suluo amesema hayo kwenye kikao kilichoshirikisha wadau wa huduma za Tiketi Mtandao, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) katika ukumbi wa mikutano wa LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Aprili 30, 2024.

 “Kwa Mamlaka tuliyonayo kwa mujibu wa Sheria, na kwa kuzingatia kuwa tumekuwa tukiwapa muda wa kutosha kwenye maandalizi ya kuunganisha mifumo yenu TRA, LATRA inatoa muda wa mwisho kwa anayetaka kusajiliwa kuwa baada ya tarehe 31 Mei, 2024, LATRA itaanza usajili wa watoa huduma waliokidhi takwa la kuunganishwa na TRA EFDMS kwa kipindi cha wiki mbili hadi kufikia tarehe 15 Juni, 2024,” amesema CPA Suluo.

Pia, amewakumbusha wamiliki kuwasiliana na timu ya ufundi ya TRA kupitia anwani ya baruapepe efdms.technical@tra.go.tz ili kupata msaada, miongozo pamoja na kukaguliwa kazi zao pindi wanapofanya marekebisho na hatimaye kupata uthibitisho wa TRA na kisha kusajiliwa LATRA kuwa mtoa huduma halali wa Tiketi Mtandao kwa mabasi nchini.

Kuhusu utaratibu wa kuunganishwa na Mfumo wa TRA EFDMS, CPA Suluo amesema, Wamiliki wa mabasi au watoa huduma wenye mifumo ya Tiketi Mtandao wanapaswa kuwasilisha maombi TRA ya kufanyiwa majaribio kwa mifumo yao ya Tiketi Mtandao na pale watakapokidhi vigezo vya TRA, watapatiwa Vyeti vya Muunganisho (Certificates & Keys) ambavyo vitawawezesha kuunganisha mifumo yao ya tiketi na ule wa TRA EFDMS katika “Live Environment”.

Kwa upande wake Bw. Rodgers Makanyo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha watoa huduma za Mifumo ya Tiketi Mtandao amesema watoa huduma za mifumo wako tayari kutekeleza agizo hilo kabla ya Mei 31, 2024 kwani changamoto waliokuwa wanapitia wamezipatia ufumbuzi katika kikao hicho.

Naye Bw. Priscus Joseph, Katibu Mkuu wa TABOA amesema, jambo la kuunganisha mifumo ya Tiketi Mtandao na EFDMS ni jambo jema kwani kuongeza ufanisi wa kulipa kodi za Serikali kutasaidia kuboresha miundombinu inayotumika kutoa huduma hizo ikiwemo ujenzi wa barabara.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo