
CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewaasa watumishi wa idara ya barabara inayoongozwa na DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA kuongeza ubunifu na juhudi katika kutekeleza majukumu yao,
Amesema hayo Februari 28, 2025 alipofungua rasmi Mkutano wa Idara ya Udhibiti Usafiri wa Barabara uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Magadu Mess, Mkoani Morogoro ukiwa na lengo la kupata mrejesho wa utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita, kufanya tathmini ya utendaji kazi wa idara hiyo na kuweka mikakati ya pamoja ili kuboresha utendaji kazi na kufikia malengo ya Mamlaka.
“Niwasihi kuongeza ubunifu katika maeneo yenu ya kazi na muendelee kutoa huduma bora kwa wateja huku mkitekeleza majukumu yenu kwa uweledi, uadilifu na ufanisi kwa kuzingatia Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (QMS) ISO 9001, na mjitathmini mnapokuwa kazini kuwa unamchango gani kwenye idara yako, tutumie akili zetu kuwa wabunifu kuleta mabadiliko chanya kwenye kazi zetu tusiogope kuzungumza, ubunifu ndio mwanzo wa mapinduzi ya maendeleo kwenye kazi,” amesema CPA Suluo.
Kwa upande wake DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA ameeleza kuwa, kukua kwa sekta ya Usafirishaji imechagizwa na maboresho yanayofanyika kwenye sekta hiyo ikiwemo ushirikishwaji baina ya wadau na matumizi ya mifumo katika utendaji kazi.
“Maboresho ya teknolojia kwenye mifumo ya usafirishaji ya LATRA yamerahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati ikiwemo Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Barabara na Reli (RRIMS), ambao kwa sasa unamuwezesha msafirishaji kupata leseni kiganjani mwake bila haja ya kufika ofisi za LATRA, Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS), Mfumo Tumizi wa LATRA App, na Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS),” amesema DCP Kahatano.
DCP Kahatano ameongeza kuwa, taswira ya Mamlaka kwa wadau wa usafirishaji inazidi kuwa bora kwa jinsi Mamlaka inavyookaa na kuzungumza na wadau hao, na LATRA ipo kwa ajili ya kuwahudumia wao ili kuboresha zaidi sekta ya usafirishaji nchini.
Naye Bi. Mwadawa Sultan, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria LATRA amewafahamisha watumishi kuhusu mwongozo wa Kanuni na Sheria za Mamlaka katika kutekeleza majukumu ya idara ya Barabara. “Katika kikao hiki tumeweza kujua na kuelewa zaidi Sheria za Mamlaka hususan kifungu cha 5 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini sura ya 413 ambayo ndio Sheria iliyounda LATRA na kimsingi inatupa jukumu la kutekeleza Sheria za kisekta,” amesema Bi Sultan.
Mkutano huo umefanyika Februari 28 hadi Machi 1, 2025 na umejumuisha wajumbe wa menejimenti ya LATRA na maafisa wote walioko chini ya idara ya Barabara LATRA kutoka mikoa yote Tanzania Bara. Mkutano huo umewawezesha maafisa hao kubadilishana uzoefu na kujadili mada mbalimbali ikiwemo mfumo mpya wa ukataji tiketi kwa njia ya mtandao SAFARI TIKETI na Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) ambapo inatajwa kurahisisha utendaji kazi za kiudhibiti.