Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA CPA DKT. HABIBU SULUO, MKURUGENZI MKUU LATRA KWENYE HAFLA YA UFUNGUZI WA MAADHIMISHO YA KWANZA YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI 2025, JNICC DAR ES SALAAM, 26 NOVEMBA, 2025
26 Nov, 2025 Pakua
  • Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Mchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mgeni Rasmi,
  • Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi na Mawaziri Mliopo,
  • Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri Uchukuzi na Manaibu Waziri Mliopo
  • Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
  • Prof. Godius W. Kahyarara, Katibu Mkuu, WU na Makatibu Wakuu Mliopo
  • Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mliopo,
  • Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam,
  • Bw. Raymond Shoniwa, Mtendaji Mkuu wa Sekretariat ya Umoja wa Reli Kusini mwa Afrika (SARA) na Wadau Wote kutoka Nje ya Tanzania
  • Viongozi wa Wizara, Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi,
  • Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho haya,
  • Viongozi na wajumbe wa vyama vya wasafirishaji mliopo,
  • Watoa Huduma za Usafiri Ardhini,
  • Watumiaji Huduma za Usafiri Ardhini na Wadau wa Sekta ya Uchukuzi,
  • Wanahabari,
  • Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana
  • Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
  •  

  • SHUKRANI
  • Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

    Kwa niaba ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutupa uhai, afya njema, na fursa ya kukutana mahali hapa ili kuadhimisha Siku ya Usafiri Endelevu Duniani 2025, na kwa mara ya kwanza kufanya maadhimisho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025 hapa Nchini.

     

    Pili, tunatoa shukrani maalum kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Uongozi Mzima wa Serikali ya Awamu ya Sita, kwa Usikivu, na Uongozi Mahiri ulioweka mazingira rafiki sana yaliyojengwa kupitia falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms, & Rebuilding) katika usimamizi wa sekta ya uchukuzi Nchini ambayo yalikuza  shughuli za kiuchumi na kijamii. Wasafirishaji wanamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuboresha mazingira ya biashara zao pamoja na kutoa ruhusa ya mabasi kusafiri usiku na mchana 24/7 baada ya zuio la miaka 20 hivyo, kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.

     

    Tatu, tunakushukuru sana wewe binafsi kwa kukukubali mwaliko wa Waziri wa Uchukuzi, kuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho haya. Tunatambua majukumu yako makubwa, hasa kipindi hiki cha baada tu ya Uchaguzi Mkuu 2025, lakini bado umeweza kutupa thamani na kuwa nasi leo. Hii inadhihirisha mapenzi makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Watoa Huduma za Usafiri Ardhini.

     

    Mwisho, sio kwa umuhimu, tunawashukuru sana Jeshi la Polisi, Watoa Huduma za Usafiri Nchini (Wamiliki wa Magari, Madereva, Wahudumu – Kondakta na Utingo, Vyuo vya Mafunzo ya Usafiri na Usafirishaji, Watoa Huduma wa Tiketi Mtandao, Watoa Huduma wa Vifaa vya Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTD), Wauza Magari ya Abiria na Mizigo, Vyama vya Wasafirishaji), Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini na Baraza lao (LATRA CCC), kwa ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu yetu, na pia kwa wote waliokuja kushiriki kwenye maadhimisho haya. Asanteni Sana!

  • UMOJA WA MATAIFA KUANZISHA SIKU YA USAFIRI ENDELEVU DUNIANI
  • Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

    Tarehe 16 Mei 2023, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio Na. 77/286 na kuteua tarehe 26 Novemba ya kila Mwaka kuwa Siku ya Usafiri Endelevu Duniani (World Sustainable Transport Day). Uamuzi huu wa kihistoria unawakilisha hatua nyingine muhimu katika kukuza ushirikiano wa usafiri endelevu na kuendeleza ahadi ya kimataifa ikijumuisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals – SDGs 2030), na Makubaliano ya Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (Paris Agreement on Climate Change) ya Mwaka 2015, ambazo zinahusu kuboresha usalama wa mazingira pamoja na usafiri duniani. Hivyo, Siku ya Usafiri Endelevu Duniani ilianza kusherehekewa kwa mara ya kwanza tarehe 26 Novemba 2023.


    Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilizikaribisha Nchi zote duniani, Taasisi za Umoja wa Mataifa, Taasisi za Kikanda na Kimataifa, Jumuiya za Kiraia, ikijumuisha Taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs), na wadau wengine wote wa usafiri na usafirishaji, kuiadhimisha siku hii kwa kutoa elimu na kuandaa shughuli zitakazokuza elimu juu ya masuala ya usafiri na usafirishaji, hususan aina za usafiri bora na salama, kuhamasisha usafiri unaotunza mazingira, kujenga miundombinu ya usafiri inayozingatia watu wenye mahitaji maalum, na masuala mengine ya usafiri bora, salama na endelevu.

     

    Ni kwa mantiki hii, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), iliamua kuandaa maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025, tarehe 24-29 Novemba 2025, sambamba na Siku ya Usafiri Endelevu Duniani ambayo ni leo, tarehe 26 Novemba 2025.

     

  • MAADHIMISHO WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI-TANZANIA
  • Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

    Tunafahamu kwamba Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Majini Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Septemba ambapo hapa Nchini, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) husimamia maadhimisho hayo chini ya miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri Baharini (IMO). Aidha, Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 07 Disemba na hapa Nchini, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) husimamia maadhimisho hayo chini ya miongozo ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).

     

    Hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na inayotambua na kuthamini maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, imeamua kuanzia mwaka 2025 madhimisho haya yafanywe kupitia Wizara ya Uchukuzi na LATRA, kwa jina la Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025 sambamba na Siku ya Usafiri Endelevu Duniani 2025.  Kauli Mbiu ya maadhimisho haya ni Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji (Green Transport and Innovation). Kauli Mbiu hii inasisitiza jukumu muhimu la mifumo ya usafiri shirikishi, yenye ustahimilivu na iliyo rafiki kwa mazingira katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi.

     

    Kwa kuzingatia ukweli kwamba ufanisi wa huduma za usafiri wa majini na usafiri wa anga vinategemeana na ufanisi wa usafiri ardhini, TCAA na TASAC ni washiriki katika maadhimisho haya. Aidha, LATRA tumeshirikiana na pacha wetu Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani ya Zanzibar (ZARTSA). Taasisi zetu hizi, LATRA, TASAC, TCAA na ZARTSA, zimeshirikiana pia katika maandalizi ya maadhimisho haya, na zote zinashiriki maonesho yanayoendelea Mnazi Mmoja.

     

    Mheshimiwa Mgeni Rasmi

    Maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025 yamefanywa na Kamati ya Pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi ikijumuisha Watoa Huduma, Watumia Huduma, na Wadau wa Usafiri na Usafirishaji, chini ya Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi.

     

    Maadhimisho haya yanajumuisha Mkutano utakaokuwa na makongamano, midahalo ya kisera, na maonesho ya kazi mbali mbali za wadau ambapo imewaleta pamoja Waoneshaji (Exhibitors) 63 katika viwanja vya Mnazi Mmoja na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani, na ukanda mzima wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye Kongamano JNICC. Mada zitakazojadiliwa zimejikita kwenye Kauli Mbiu ya Maadhimisho haya. Aidha, washiriki zaidi ya 6,000 wanatarajiwa kuhudhuria maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Vilevile, siku ya tarehe 28 Novemba 2025, kutakuwa na utalii mfupi kwa washiriki kusafiri kwa SGR (EMU-Mchongoko), kutoka Dar es Salaam (KM 0) kwenda Kituo cha Kwala na Kurudi Dar es Salaam (KM 0).

     

    Mheshimiwa Mgeni Rasmi

    Maadhimisho haya yamewezekana kwa kuwezeshwa na Wadhamini zaidi ya 30 waliojitolea muda wao na rasilimali fedha. Naomba niwatambue mbele yako na kuwashukuru sana wadhamini wetu wote, na shukrani maalum kwa wadhamini wa makundi yafuatayo:                                                                                                                                                        Soma zaidi

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo