Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHE. ALBERT JOHN CHALAMILA - MKUU WA MKOA DAR ES SALAAM KWENYE HAFLA YA KUKABIDHI CHETI CHA UWAKALA WA KUTOA LESENI ZA USAFIRISHAJI KWA MAUPIDA SACCOS LTD AGOSTI 13, 2025
13 Aug, 2025 Pakua

Tarehe: 13 Agostii, 2025

Mahala: Ukumbi wa Mikutano wa Golden Jubilee, Dar es Salaam.

 

  • Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam
  • Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,
  • Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania
  • Ndugu Viongozi wa Kiroho ambao ni wadau Muhimu wa MAUPIDA SACCOS LTD
  • Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo,
  • Menejimenti ya LATRA Mliopo,
  • Wadau mbalimbali wa sekta ya Usafirishaji,
  • Viongozi na wanachama wa Shirikisho la vyama vya wamiliki na waendesha Pikipiki
  • Viongozi na wanachama wa MAUPIDA SACCOS LTD,
  • Wadau wa Usafiri Ardhini,
  • Ndugu Wanahabari,
  • Wageni waalikwa, mabibi na mabwana, Itifaki imezingatiwa,

 

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA…

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai, afya na kuibariki Serikali yetu ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia nashukuru kwa heshima niliyopewa na LATRA ya kuwa mgeni Rasmi katika hafla hii ya kukabidhi Cheti cha Uwakala wa Kutoa Leseni za Usafirishaji kwa Chama cha Kuweka na Kukopa Ushirika cha Maafisa Usafirishaji wa Pikipiki mkoa wa Dar es salaam (MAUPIDA SACCOS LTD). Pia, nafahamu kuwa Aprili 04, 2025 Mhe. Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, alikabidhi cheti cha ushirika kwa chama hiki cha MAUPIDA SACCOS LTD kufuatia jitihada nyingi alizozifanya za kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa Ushirika huu unaanzishwa.

 

Ndugu viongozi, na wageni waalikwa,

Sote ni mashahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi Mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya juhudi za kipekee za kuhakikisha huduma za usafirishaji zinaboreshwa, zinakuwa salama na zinachangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi na kijamii,

 

Ndugu viongozi, na wageni waalikwa,

Rais wetu anatambua juhudi za maafisa usafirishaji katika kuimarisha uchumi wao na nchi kwa jumla na  ndio maana anafanya jitihada za dhati za kuhakikisha vijana na wadau wote wanaokuwa katika sekta hii ya usafiri wanajikwamua kiuchumi na kijamiii kwa kufungua fursa mbalimbali na kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya kufanya biashara. Moja ya jitihada ambazo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayofanya ni kupitia kuwawezesha maafisa wasafirishaji kufanya shughuli zao kupitia ushirika ambao utawaweka karibu wanaushirika na hivyo kuwasaidia katika masuala ya kijamii na kiuchumi.

 

Ndugu viongozi, na wageni waalikwa,

Serikali yetu sikivu ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozo Mahiri wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahamasisha kuundwa kwa vyama vya

 

ushirika vya watoa huduma za usafiri kama mkakati madhubuti wa kuwawezesha wadau hawa kushirikiana, kupata mikopo kwa urahisi, kuongeza nguvu ya sauti yao katika maamuzi, kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi na kuzingatia uweledi na kurahisisha uratibu wa shughuli zao. Ushirika unarahisisha utekelezaji wa Sera, Sheria na Mifumo ya kisasa ya usimamizi wa sekta ya usafiri.

 

Ndugu viongozi, na wageni waalikwa,

Niwapongeze sana maafisa wasafirishaji mkoa wa Dar es Salaam kwa kuungana pamoja na kupata wazo la kuunda chama cha ushirika cha kuweka na kukopa (SACCOS). Niwahakikishie kwamba mmefanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwa sababu kupitia ushirika mtakuwa wamoja, mtashirikiana sio tu katika masuala ya kazi lakini pia mtakuwa karibu zaidi kijamii.

 

Ndugu viongozi, na wageni waalikwa,

Serikali kupitia kanuni za LATRA itawawezesha MAUPIDA SACCOS LTD kiuchumi kwa kutoa gawio la asilimia 20 ya makusanyo ya ada za leseni za usafirishaji watakazoweza kutoa kwa mujibu wa Cheti cha uwakala watakachokabidhiwa siku ya leo. Tutoe pongezi nyingi kwa LATRA kwa

 

kuwezesha jambo hili kwa wadau wake ambalo litakwenda kuwanufaisha watoa huduma walioungana katika ushirika kama walivyofanya MAUPIDA SACCOS LTD. Nawasihi sana mkatumie vizuri ili iwaletee maendeleo kwa kufanya vitu mbalimbali kama vile kufungua miradi mbalimbali itakayosaidia kuwainua kiuchumi. Serikali yenu, itaona fahari kubwa mkiwa mtafikia malengo mliyojiwekea hivyo viongozi na wanachama mnapaswa kuwa wamoja na kuhakikisha malengo mliyojiwekea yanatimia kupitia uwakala wenu.

 

Ndugu viongozi, na wageni waalikwa,

MAUPIDA, sasa mmekuwa mawakala rasmi wa LATRA, mna jukumu kubwa la kuhamasishana kufanya kazi zenu kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizopo ikiwemo la kila chombo kinachotoa huduma ya usafirishaji katika kundi lenu inakuwa na leseni ya usafirishaji na kufuata masharti yake huku mkizingatia usalama wenu na abiria mtakaowabeba. Muhimizane ninyi kwa ninyi kufuata alama za barabarani, kuendesha kwa mwendo unaokubalika kwa mujibu wa Sheria, epukeni kufanya vitendo vinavyohatarisha maisha yenu mkiwa katika kazi zenu na kikubwa zaidi mkumbuke kuwa ninyi ni nguvukazi ya Taifa lakini pia mnategemewa na familia zenu, hivyo usalama unatakiwa kuwa kipaumbele chenu.

 

Ndugu viongozi, MAUPIDA na wageni waalikwa,

Mkoa wa Dar es Salaam utaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa LATRA, MAUPIDA SACCOS LTD pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha shughuli za usafirishaji zinafanyika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na miongozo iliyopo. Tunataka kuona Pikipiki magurudumu mawili na matatu (maafrufu kama Bodaboda na Bajaj), Daladala, na watoa huduma wengine wa usafiri Ardhini wakifanya kazi katika mazingira yenye mpangilio mzuri, usalama na tija kwa jamii na taifa kwa jumla.

 

Ndugu viongozi, MAUPIDA SACCOS LTD na wageni waalikwa,

Kipekee kabisa nimpongeze CPA Habibu Juma Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA, Menejimenti na watumishi wote wa Mamlaka hii kwa kutekeleza maono ya Mhe. Rais kwa vitendo. Ninamefuatilia na nimebaini kuwa Ushirika kama huu tayari umeanzishwa na imeonesha matokeo chanya katika baadhi ya mikoa ikiwepo Kilimanjaro, Mwanza, Arusha, na ninatamani wamiliki na waendesha pikipiki (Maafisa wasafirishaji) katika maeneo mengine waige mfano huu wa kuanzisha  ushirika ili wakidhi vigezo vya kupatiwa hadhi ya uwakala wa LATRA kwa sababu manufaa ni mengi.

 

Mimi niwahakikishie tu kuwa, juhudi hizi mnazozifanya haziendi bure bali zinaenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri ardhini hapa nchini kwa kuwa tunaenda kuona waendesha pikipiki magurudumu mawili na matatu (Maafisa Usafirishaji) wakiwa na maendeleo.

 

 Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 

Mhe. Albert John Chalamila

MKUU WA MKOA - DAR ES SALAAM

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo