- CPA Habibu J. Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,
- DCP Ramadhani Ng’anzi, Kamanda wa Polisi - Kikosi cha Usalama Barabarani,
- Dkt. Zainab Rashid, Mwenyekiti wa Kamati ya Uthibitishaji Madereva-LATRA
- Ndugu Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo hapa,
- Ndugu Wenyeviti na Viongozi wa Vyama vya Madereva na Wasafirishaji ikiwemo CHAWAMATA, TADWU, UWAMATA, TATOA, TAT, TAMSTOA, TRFA, DARCOBOA NA UWADAR,
- Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa
- Ndugu wanahabari,
- Wageni waalikwa, mabibi na mabwana, Itifaki imezingatiwa,
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA…
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai, afya na kuibariki Serikali yetu ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia nashukuru kwa heshima niliyopewa na LATRA ya kuwa mgeni Rasmi katika hafla hii ya utoaji wa vyeti kwa madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma ya usafiri kibiashara waliofanya mtihani na kuthibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA). Nimeambiwa kuwa, hii ni hafla ya pili kwa madereva ambapo mara ya kwanza ilifanyika Julai 01, 2023 ambapo LATRA ilitoa vyeti kwa madereva 999.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Sote ni mashahidi kuwa Serikali ya awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya juhudi za kipekee za kuhakikisha suala la ajali linapungua nchini kama si kumalizika kabisa. Rais wetu anatambua kuwa ajali ni mwiba kwa kuwa zimekuwa zikipoteza nguvukazi ya Taifa, huku wengine wakiachwa bila wazazi na wengine kupata ulemavu wa maisha. Jambo hili linamnyima usingizi Rais wetu na ndio maana anafanya kila linalowezekana kuhakikisha suala hili linapungua au hata kwisha kabisa.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Bila shaka tunatambua kuwa takwimu hapa nchini zinaonesha zaidi ya zaidi ya asilimia 76 ya ajali zinazotokea barabarani zinachangiwa na makosa ya kibinadamu wakati asilimilia 24 iliyobakia inachangiwa na ubovu wa magari (16%) na mazingira ya barabara (8%). Nitumie nafasi hii Kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa LATRA kwa kuwa na Kitengo cha Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Hudumu wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara kwa ajili ya kuwasimamia madereva na wahudumu wao.
Pia, Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza sana suala la ushirikishaji wa wadau katika kutekeleza majukumu ya taasisi, kwa hili pia LATRA wamelitekeleza kwa vitendo na tumeona kuwa wameshirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo Jeshi la Polisi, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), madereva wenyewe na wadau wengine, kuandaa kwa pamoja maswali yenye nia njema ya kufahamu uelewa wa madereva wetu. Lengo ni zuri tu la kuwapika madereva wetu ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na ufanisi huku wakizingatia suala la usalama barabarani.
Lakini niwapongeze pia LATRA kwa kuandaa Mtaala wa Mafunzo Mafupi ya Wahudumu wa Mabasi kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), na kuanza kuwasajili wahudumu wa mabasi kwa mujibu wa Sheria ya LATRA na Kanuni zake. Jambo hili linafanya huduma za usafiri wa abiria hasa wa mabasi ya mikoani iboreke zaidi na iwe ya viwango vya juu. Hongera sana, endeleeni na kazi nzuri na msiwasahau na wahudumu (makondakta) wa Daladala hasa wa Jiji hili la Dar es Salaam,
Mimi niwahakikishie tu kuwa, juhudi hizi mnazozifanya haziendi bure bali zinaenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri ardhini hapa nchini kwa kuwa mabadiliko ya tabia za madereva wakiwa barabarani yatakuwa ni yenye kuridhisha na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali nchini.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Imeelezwa hapa na Mkurugenzi Mkuu kwamba, kuanzia tarehe 01 Juni, 2023 hadi 31 Machi, 2024 jumla ya madereva 8,729 wamesajiliwa kwenye kanzidata ya LATRA, ambapo kati yao, madereva 3,254, sawa na asilimia 37.3, wamejitokeza kufanya mitihani na leo hii tunaenda kuwatunuku vyeti madereva waliothibitishwa na LATRA. Ninawapongeza sana kwa hatua hii muhimu, msikatishwe tamaa na idadi hii, lakini pia muendelee kuwahimiza madereva wajitokeze kwa wingi zaidi na waweze kujisajili kwa wingi na hatimaye wafanye mitihani na kuthibitishwa na LATRA.
Nanyi ndugu zangu madereva mliofaulu mitihani na kuthibitishwa na LATRA, niwahakikishie kuwa, kama alivyoeleza Mkurugenzi Mkuu, vyeti mtakavyotunukiwa leo vitatambulika kitaifa na kimataifa hasa kwa Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), haya ni manufaa makubwa kwa kuwa mnaenda kutanua wigo wa ajira ndani na nje ya nchi yetu na hivyo mtajiinua kiuchumi na kijamii.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Suala la uthibitishaji wa madereva lina faida nyingi ikiwemo kupata kumbukumbu ya mwenendo wa dereva katika kazi hasa Kampuni alizopitia, kuwezesha wamiliki wa magari kuwa na madereva wenye weledi na nidhamu, kusaidia upatikanaji wa madereva mahiri, kuwawezesha madereva kutambulika na kupatiwa mikataba ya ajira, kusaidia madereva kujikumbusha mambo waliyosoma darasani pamoja na kuitangaza Nchi yetu duniani kwa namna madereva wanavyokuwa weledi.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawathamini sana na imedhamiria kuongeza hadhi ya madereva na ndio maana kupitia LATRA jambo hili linafanyika. Uthibitishaji huu wa madereva utawaheshimisha zaidi na maslahi yenu yataboreshwa na zaidi ya yote, taaluma hii ya udereva itarasimishwa na kukomesha tabia ya baadhi ya wasafirishaji kuwapa kazi ya udereva watu wasiostahili kufanya kazi hiyo.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Naomba nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Mhe. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuiwezesha LATRA kutekeleza jukumu hili ambalo ni muhimu kwa mujibu wa sheria. Pia, nawasihi wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi hizi za Serikali ukizingatia ukweli kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za usafirishaji kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Ndugu viongozi, madereva na wageni waalikwa,
Kwa hayo machache, napenda kutamka kuwa nimefungua rasmi hafla hii na sasa nipo tayari kwa ajili ya jukumu la na kutoa vyeti kwa madereva waliofanya mtihani na kuthibitishwa na LATRA.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Mhe. Albert John Chalamila
MKUU WA MKOA-DAR ES SALAAM