Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHESHIMIWA DAVID KIHENZILE (MB) – NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI KATIKA HAFLA YA UTOAJI WA KADI KWA WAHUDUMU WA MABASI YA ABIRIA WALIOHITIMU MAFUNZO NA KUSAJILIWA NA LATRA
12 Nov, 2024 Pakua
  • Prof. Mohamed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi LATRA,
  • DCP Johansen Kahatano, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu LATRA;
  • Viongozi wengine wa LATRA;
  • Mwakilishi kutoka Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu Kimtandao (National Internet Data Centre);
  • Ndugu Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo hapa mkiongozwa na NIT, CBE, NIDC
  • Ndugu Wenyeviti na Viongozi wa Vyama vya Madereva na Wasafirishaji ikiwemo, TABOA, DARCOBOA NA UWADAR,  
  • Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa;
  • Ndugu wanahabari,
  • Wageni waalikwa, mabibi na mabwana.

 

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA!- Shukran

  1. Namshukuru Mwenyezi MUNGU mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai, afya na kuibariki Serikali yetu ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  2. Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
  3. Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
  4. Mhe. Dotto Mashaka Biteko (Mb),  Naibu Waziri  Mkuu wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania;
  5. Mhe. Prof. Makame M. Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi kwa kuendelea  kusimamia vizuri Wizara na Taasisi zake.
  6. Pia nashukuru kwa heshima niliyopewa na LATRA ya kuwa mgeni Rasmi katika hafla hii ya kukabidhi kadi za utambuzi kwa wahudumu wa mabasi ya abiria waliokidhi vigezo baada ya kupata mafunzo, kufaulu na kusajiliwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

Ndugu wageni waalikwa,

Ndugu wageni waalikwa,(Pongezi)

  1. Bodi na Menejimenti ya LATRA kwa kuhakikisha suala la ubora wa huduma za usafiri linapewa kipaumbele na uzito wa kipekee na kusimamamia ushirikishwaji wa wadau katika kutekeleza majukumu ya taasisi. Mathalani katika hili, Aidha, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya LATRA kwa kuanzisha kituo cha Uthibitishaji Madereva na Usajili wahudumu wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara.  Kituo hiki ni kwa ajili ya kuwasimamia madereva na wahudumu wa vyombo husika katika jitihada za kuboresha utendaji wao. Natambua kuwa, mchango wa madereva katika eneo la usalama barabarani ni zaidi ya asilimia 70 na hivyo, weledi wao una umuhimu wa kipekee katika usimamizi wa usalama wa huduma.
  2. Bodi na Menejimenti ya LATRA kwa kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo Kituo Cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kuandaa mafunzo yenye lengo la kupata wahudumu wenye sifa na NIDC kutengeneza kadi za utambuzi wa wahudumu.

Niwahakikishie tu kuwa, juhudi hizi mnazozifanya haziendi bure bali zinaenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri ardhini hapa nchini kwa kuwa mabadiliko ya tabia za wahudumu na madereva wakiwa barabarani yatakuwa ni yenye kuridhisha na hivyo kuchangia kuboresha huduma za usafiri na kupunguza ajali nchini.

 

Ndugu wageni waalikwa,

Nimetaarifiwa kuwa, kuanzia Mwezi Novemba, 2023 hadi Oktoba, 2024 zaidi ya wahudumu 750 wamepata mafunzo kutoka vyuo vya NIT na CBE, katika kipindi hicho jumla ya wahudumu 254 wamesajiliwa kwenye kanzidata ya LATRA na leo wahudumu waliokidhi vigezo na kupewa kadi ni 174 ambao miongoni mwao wahudumu 100 watapatiwa kadi za kusajiliwa na Mamlaka. Ninawapongeza na kuwasihi LATRA kuhakikisha kuwa wahudumu wote wajitokeze kupata mafunzo na kusajiliwa na LATRA.

Ndugu zangu wahudumu mnaokabidhiwa kadi zenu leo, nawapongeza sana! Ninawasihi kuwa mfano bora kwa wengine.  Niwahakikishie kuwa kadi hizi za utambuzi zitasaidia kurasimisha ajira zenu ili ziheshimike kama zilivyo kazi zingine, kuboresha vipato vyenu kwani thamani yenu kwenye soko la ajira ya usafirishaji itaongezeka.  Vilevile kadi hizi zitawezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowezesha kusimamia maslahi ya wahudumu.

Nitoe wito kwenu kuwa pamoja na jitihada hizi zinazoendelea kufanyika za kutoa mafunzo kwa wahudhumu tuongeze nguvu zaidi kwenye utoaji elimu kwa watumiaji waote wa mindombinu ya barabara ili kupunguza vifo vinavyotokea kupitia usafiri wa mabasi nchini.

Ndugu wageni waalikwa,

Nimetaarifiwa kuwa, wapo baadhi ya wahudumu wakati wakipata mafunzo haya, waajiri wao waliwaachisha kazi na kuajiri wahudumu wasiokuwa na mafunzo.  Nipende kutoa rai kwa watoa huduma wote nchini kuacha vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma jitihada za Serikali na za sekta binafsi katika kuboresha huduma za usafiri nchini.  Aidha, niwawasititize wahudumu wa mabasi nchini watumie fursa hii adhimu  kujiunga na mafunzo haya ya muda mfupi bila ya kuwa na wasiwasi wowote.

Ndugu wageni waalikwa,

Siku hii ya leo ni muhimu sana katika historia ya Nchi yetu na hususan Sekta ya Uchukuzi kwani kwa mara kwanza tunashuhudia LATRA ikitekeleza kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 iliyopitishwa na Bunge la Tanzania Mwaka 2019 na Kanuni za Uthibitishaji wa Madereva na Usajili wa Wahudumu za Mwaka 2020 kwa kuwezesha mafunzo ya Wahudumu wa Mabasi nchini. Natoa kongole kwa wote  waliofanikisha  suala hili.

Ndugu wageni waalikwa,

Kwa hayo machache, napenda kutamka kuwa  hafla hii  imefunguliwa rasmi. Sasa nipo tayari kutoa kadi kwa wahudumu wote waliosajiliwa baada ya kupata mafunzo, kufaulu mtihani katika vyuo vya NIT na CBE na baadaye kusajiliwa na LATRA.

 

Asanteni kwa kunisikiliza

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo