Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU – LATRA KWENYE HAFLA YA KUKABIDHI CHETI CHA UWAKALA WA KUTOA LESENI ZA USAFIRISHAJI KWA MAUPIDA SACCOS LTD AGOSTI 13, 2025
13 Aug, 2025 Pakua

Tarehe: 13 Agosti, 2025  

Mahala: Ukumbi wa Mikutano wa Golden Jubilee, Dar es Salaam.

  • Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam
  • Mhe. Albert John Chalamila, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam,
  • Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania
  • Ndugu Viongozi wa Kiroho ambao ni wadau Muhimu wa MAUPIDA SACCOS
  • Ndugu Viongozi wa Benki Mbalimbali ambao ni wadau Muhimu wa MAUPIDA SACCOS
  • Ndugu Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo,
  • Wajumbe wa Menejimenti ya LATRA,
  • Wadau mbalimbali wa sekta ya Usafirishaji,
  • Viongozi na wanachama wa Shirikisho la vyama vya wamiliki na waendesha Pikipiki
  • Viongozi wa Bodi na wanachama wa Chama cha Ushirika Cha Kuweka na Kukopa Cha Maafisa Usafirishaji wa Pikipiki mkoa wa Dar es salaam (MAUPIDA SACCOS),
  • Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa,
  • Ndugu wanahabari,
  • Wageni waalikwa, mabibi na mabwana, Itifaki imezingatiwa,

    

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA…

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uhai, afya njema na fursa ya kukutana tena leo kwenye hafla hii ya kukabidhi Cheti cha Uwakala wa Kutoa Leseni za Usafirishaji kwa niaba ya LATRA kwa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Maafisa Usafirishaji wa Pikipiki mkoa wa Dar es salaam (MAUPIDA SACCOS LTD).

 

Pili, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi - LATRA, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), natoa shukrani za dhati kabisa kwako wewe Mhe. Albert John Chalamila, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam kwa kukubali mwaliko wetu wa kuwa Mgeni Rasmi na kuja kuhudhuria hafla hii na kuwakabidhi Cheti cha Uwakala wa LATRA kwa Chama Cha Kuweka na Kukopa cha Maafisa Usafirishaji kwa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (MAUPIDA SACCOS LTD)

 

Tunafahamu kuwa, una majukumu mengi ya nafasi yako, na tunatambua kuwa siku ya leo ulikuwa na ratiba nyingine muhimu lakini umeweza kuipa thamani siku hii na kuja mwenyewe kujumuika nasi. Tunakushukuru sana.

 

Pia, Mhe. Mgeni Rasmi, tunakushukuru wewe binafsi na Ofisi yako kwa kuendelea kushirikiana na LATRA katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali za usafirishaji katika jiji hili la Dar es Salaam. Tunafahamu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapendezwi na hali ya huduma ya usairi  ilivyo lakini kupitia Serikali yake ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake mahiri, ameshatoa maelekezo  ya kutatua changamoto zilizopo. Kwa upande wa usafiri ardhini, Mhe. Rais ameendelea kuiwezesha LATRA kwa rasilimali zote zinahitajika kwa ajili ya kutekeleza majukumju yake yote ya kuhakikisha kuwa huduma za usafiri na usafirishaji zinapatikana kwa watanzania wote.

 

Vilevile, tunamshukuru sana Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Prof. Godius W. Kahyarara, Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi na Bw. Ludovick Nduhiye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi pamoja na Menejimenti nzima ya Wizara ya Uchukuzi kwa namna wanavyotuongoza na kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania ikijumuisha watoa huduma na watumia huduma tunazodhibiti.

 

Mwisho, lakini kwa umuhimu mkubwa kabisa, naomba kutumia fursa hii kutoa shukrani maalum kwa wasafirishaji wote wanaotumia barabara hasa wale tunaowadhibiti kwa kuendelea kushirikiana na Mamlaka na kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama Barabarani.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Katika kutimiza maono ya Mhe. Rais Dkt, Samia ya kuongeza fursa za kiuchumi kwa wasafirishaji nchini, LATRA kwa sasa tunafanya jitihada kubwa ya kuwaunganisha pamoja maafisa wasafirishaji kwa kuwapatia elimu na kuwashawishi wajiunge na kuanzisha vyama vya ushirika ambavyo vitawasaidia kuwa na umoja wa kusaidiana na kuweka akiba kwa kuwaongezea kipato na hatimaye kujiinua kiuchumi na kijamii.

 

Vilevile, LATRA inalenga kuondoka kwenye utaratibu wa kudhibiti mtu mmoja mmoja na kwenda kwenye mfumo wa udhibiti kupitia vyama vya ushirika au kampuni (Self-Regulation) ambapo wasafirishaji watainuana kiuchumi lakini pia watakuwa wanasimamiana kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria na utaratibu uliopo huku wakizingatia masharti ya leseni za usafirishaji walizonazo bila kushurutishwa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

 

Tarehe Aprili 04, 2025 Mhe. Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, alikabidhi cheti cha ushirika kwa chama hiki cha MAUPIDA SACCOS LTD baada ya kukamilisha taratibu zote zilizohitajika na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC). Leo tunaenda kushuhudia MAUPIDA SACCOS LTD wakikabidhiwa cheti cha Uwakala wa kutoa leseni za usafirishaji kwa niaba ya LATRA, Mamlaka inawapongeza sana MAUPIDA SACCOS LTD kwa hatua hii muhimu waliyofikia na tunawasihi wakawe waaminifu katika kazi hii wanayoenda kuifanya lakini pia wawe mstari wa mbele kuhamasishana kufanya kazi zao kwa uweledi, ufanisi huku wakizingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

 

Cheti cha Uwakala utakachowakabidhi leo kitaruhusu MAUPIDA SACCOS kutoa aina sita za leseni za vyombo vya moto vya kukodi ambazo  ni  leseni za Pikipiki za Magurudumu Mawili,   Leseni za Pikipiki za Magurudumu Matatu, Leseni za Taksi za kawaida, Leseni za Taksi Mtandao(Ride Hailing), Leseni za Magari Maalumu ya Kukodi (Special Hire) pamoja na Leseni za Kuitisha Mtandaoni Usafiri wa Kuchangia (Ride Sharing).

Pia, ili kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendelea kusimama na kuwanufaisha walengwa, Mamlaka inatoa asilimia ishirini (20%) kila mwezi kama gawio linalotokana na ada ya leseni zitakazolipwa, hivyo nawasihi MAUPIDA SACCOS kujituma zaidi ili waweze kutoa leseni nyingi na hatimaye kunufaika zaidi na gawio ambalo tunaamini linaenda kuwainua kiuchumi kwa kubuni na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo huku wakitoa huduma bora na salama za usafiri kwa wananchi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

LATRA pamoja na Shirikisho la vyama vya wamiliki na waendesha Pikipiki magurudumu mawili na matatu katika mkoa wa Dar es Salaam, tumekuwa na ushirikiano wa karibu sana katika maeneo mbalimbali, ikiwepo hili la wao kuwezeshwa kuwa wakala wetu wa kutoa leseni za usafirishaji kwa niaba yetu, Matumizi ya sare maalum kwa madereva wa pikipiki pamoja na kuwawezesha wao kutumia mfumo wa LATRA, pia tupo katika hatua nzuri ya kuwezesha mfumo wao wa Tehama kusomana na mfumo wetu ili kurahisisha ushirikiano wa taarifa na kuweka kumbukumbu za pamoja zitakazotumika katika usimamizi wa vyombo husika.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Tunachukua fursa hii kutoa shukrani zetu za dhati kwa Wakuu wa mikoa mitatu kwa kuunga mkono jitihada za Mamlaka za uanzishwaji wa SACCOS za waendesha Pikipiki katika mikoa yao; Mhe. Nurdin Babu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwezesha kuanzishwa kwa SACCOS ya kwanza ya Kilimanjaro Bajaji na Bodaboda (KIBABOT) iliyosajiliwa tarehe 03 Agosti 2023, na kupatiwa cheti cha Uwakala wa LATRA tarehe 26 Februari 2024, Mhe. Said Mtanda, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa kuwezesha kuanzishwa kwa SACCOS ya Pili ya Ushirika wa Wasafirishaji Mwanza (UWAMWA) iliyosajiliwa tarehe 04 Februari 2025, na kupatiwa cheti cha Uwakala wa LATRA tarehe 24 Juni, 2025, na wewe Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwezesha kuanzishwa kwa SACCOS ya tatu ya Maafisa Usafirisshaji Kwa Pikipiki Dar es Salaam (MAUPIDA) iliyosajiliwa tarehe 02 Aprili 2025, na kukabidhiwa cheti cha Uwakala wa LATRA leo tarehe 13 Agosti 2025. Zipo jitahada zinazoendelea katika mikoa mbalimbali za kuhakikisha kuwa vyama hivi vya Ushirika kwa waendesha pikipiki zinaanzishwa kwa lengo la kuwawezesha kuungana kwa pamoja na kuwa katika ushirika unaoweza kushiriki katika fursa zilizopo hususan zinazotolewa na serikali.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

 

Mwisho kabisa, niwaahidi Watanzania wenzangu na Viongozi wetu na watoa huduma katika sekta tunazozidhibiti kwamba, LATRA tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa weledi, uadilifu, ubora zaidi na kujali zaidi wateja wetu wote bila upendeleo na tutatekeleza Sheria, Taratibu na Kanuni tulizokabidhiwa. Aidha, tutazingatia falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuild) ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kutekeleza majukumu yetu.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima naomba sasa nikukaribishe uongee na hadhara hii, kisha nakuomba utekeleze jukumu kubwa la kukabidhi Cheti cha Uwakala wa Kutoa Leseni za Usafirishaji kwa Chama Kuweka na Kukopa Cha Maafisa Usafirishaji kwa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (MAUPIDA SACCOS LTD).

Mheshimiwa Mgeni Rasmi naomba kuwasilisha

 

CPA Habibu J. Suluo

MKURUGENZI MKUU LATRA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo