- Mhe. Albert John Chalamila, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, na Mgeni Rasmi wa Shughuli hii;
- DCP Ramadhani Ng’anzi, Kamanda wa Polisi - Kikosi cha Usalama Barabarani;
- Dkt. Zainab Rashid, Mwenyekiti wa Kamati ya Uthibitishaji Madereva – LATRA;
- Menejimenti ya LATRA na Wasimamizi wa Mitihani mliopo;
- Ndugu Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo;
- Ndugu Wenyeviti na Viongozi wa Vyama vya Madereva na Wasafirishaji mliopo - CHAWAMATA, TADWU, UWAMATA, TATOA, TAT, TAMSTOA, TRFA, DARCOBOA NA UWADAR;
- Ndugu Madereva Mliofaulu na Kuthibitishwa na LATRA mliopo;
- Ndugu Wadau wetu mbalimbali mliojumuika nasi hapa;
- Ndugu wanahabari,
- Wageni waalikwa, mabibi na mabwana, Itifaki imezingatiwa,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uhai, afya njema na fursa ya kukutana tena leo ikiwa ni Hafla ya Pili ya kuwatambua, kuwapongeza na kuwatunuku vyeti madereva 1,518 waliofanya mitihani ya kuthibitishwa na kufaulu katika kipindi cha kuanzia tarehe 01 Juni, 2023 hadi 31 Machi, 2024. Hafla ya kwanza ilifanyika tarehe 01 Julai, 2023 katika ukumbi huu ambapo madereva 999 walitunikiwa vyeti vya kuthibitishwa na LATRA. Hivyo, katika hafla hii ya pili, tunafikisha idadi ya madereva 2,517 waliothibitishwa na LATRA.
Pili, naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za moyoni na kipekee kabisa kwako Mhe. Albert John Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kuhudhuria Hafla hii ukiwa Mgeni Rasmi. Tunafahamu majukumu ya nafasi yako, na tunatambua kuwa siku ya leo ulikuwa na ratiba nyingine muhimu pia lakini umeweza kuipa thamani hafla hii na kuja mwenyewe kujumuika nasi. Tunakushukuru sana.
Tatu, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), natoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuendelea kuwa Serikali sikivu kwa Wananchi wake na kuweka mazingira bora na rafiki kwa Sekta Binafsi, ambao wengi ndio watoa huduma wa usafiri wa barabara tunaoudhibiti. Utendaji mahiri wa Mhe. Rais wetu unatambulika na nkuheshimika kimataifa pia. Na hapa nampongeza sana Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kutunikiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu cha Anga cha Korea (Korea Aerospace University) tarehe 03 Juni 2024.
Nne, tunamshukuru sana Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Prof. Godius W. Kahyarara, Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi na Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi na Menejimenti nzima ya Wizara ya Uchukuzi kwa namna wanavyotuongoza na kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Watanzania ikijumuisha watoa huduma na watumia huduma tunazodhibiti.
Mwisho, lakini kwa umuhimu mkubwa kabisa, naomba kutumia fursa hii kutoa shukrani maalum kwa madereva waliofanya mitihani ya kuthibitishwa na LATRA; lakini, kipekee kabisa, nawapongeza wote waliofanya mitihani na kufaulu na kustahili kupewa vyeti vya kuthibitishwa. Katika kuwashukuru na kuwapongeza madereva hawa, mafanikio yao yanatokana na utashi wa wamiliki wa magari wanayoyaendesha ambao wamewatia moyo, wamewahimiza na wengine wamewalipia gharama (ada ya mitihani, nauli/usafiri na masurufu) kuhudhuria mitihani. Hongera sana kwa wote.
Niwaahidi Watanzania wenzangu na Viongozi wetu kwamba LATRA tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa weledi, uadilifu, ubora zaidi na kujali zaidi wateja wetu wote bila upendeleo na tutatekeleza Sheria, Taratibu na Kanuni tulizokabishiwa. Aidha, tutazingatia falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuild) ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kutekeleza majukumu yetu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kazi unayoiongoza hapa leo ni sehemu ya utekelezaji wa kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya LATRA iliyotupa jukumu la Kuthibitisha Madereva na Kusajili Wahudumu wa Vyombo vya Moto Kibiashara. Kwetu sisi ni siku muhimu sana na ya kihistoria kwa kuwa tunaendelea na tunashuhudia moja katika mafanikio yetu katika kutekeleza Sheria na Kanuni tulizokabidhiwa na Serikali ili kuzitekeleza.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mhe. Waziri mwenye dhamana ya Sekta ya Uchukuzi aliidhinisha Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili wa Wahudumu wa Vyombo vya Moto Kibiashara zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 81 la tarehe 7 Januari, 2020. Kufikia mwezi Mei, 2020, LATRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ilikamilisha utengenezaji na usimikaji Mfumo wa Kutahini Madereva (Drivers Testing System-DTS) wa magari yanayotoa huduma kibiashara. Hivyo, Mamlaka ilianza rasmi kusajili madereva mwezi Disemba, 2020 kwa lengo la kuwathibitisha kwa kutumia mfumo wa DTS.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kuwaandaa madereva kufanya mitihani ya kuthibitishwa na LATRA, na kwa kutambua kuwa walishafanya mitihani katika vyuo vya udereva na kufaulu, LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, tumeandaa video za kuwakumbusha madereva kuhusu masuala ya msingi ya kuzingatia ukiwa barabarani ikiwemo suala la alama na michoro. Video hizi zinapatikana katika mitandao hususan LATRA Online TV inayopatikana kwa jina la LatraTV kwenye mtandao wa YouTube. Tunawasisitiza madereva wetu watembelee mtandao huo na kujielimisha zaidi au kujikumbusha, hata kama umeshapata cheti cha kuthibitishwa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Madereva hujisajili kwa njia ya mtandao (online) kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Utoaji Huduma za Barabara na Reli (RRIMS –Railway and Road Information Management System) akiwa na NIDA, Leseni ya Udereva na Cheti cha Mafunzo ya Udereva. Awe na umri kati ya miaka 25 na 60. Kupitia mfumo wa DTS, dereva anafanya mtihani kwa njia ya kompyuta – maswali 100 kwa masaa 3 - na baada ya kumaliza kujibu maswali atawasilisha mtihani wake (online submission), utasahihishwa kielektroniki (online) na atapokea matokeo ya mtihani kwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno – SMS kupitia simu yake ya kiganjani. Alama ya ufaulu ni 70%.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Mchakato wa utoaji wa vyeti vya uthibitishaji wa madereva unaratibiwa na Kamati ya Uthibitishaji (Certification Committee) yenye wajumbe watano (5) wanaoteuliwa na Mamlaka kwa mujibu wa kanuni ya 6(1) ya Kanuni za LATRA za Uthibitishaji wa Madereva na Usajili Wahudumu Magari ya Biashara za mwaka 2020. Hivyo, Mamlaka iliunda Kamati ya Uthibitishaji madereva yenye wajumbe watano ambao Mwenyekiti wake ni Dr Zainabu Rashid na Makamu wake ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mstaafu na Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani DCP. Mohamed Mpinga. Wajumbe wengine ni Bw. Hans Tomas Mwaipopo, Bw. Venance Adamsom Mwanyumba na Bi, Faustina Ndunguru kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani. Uteuzi wa Wajumbe hawa ni kwa kipindi cha miaka mitatu (3) kwa mujibu wa kanuni ya 6(2) ya GN 81 na wanaweza kuteuliwa kwa kipindi kingine kimoja tu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kipindi cha kuanzia tarehe 01 Juni, 2023 hadi 31 Machi, 2024 tulisajili jumla ya madereva 8,729 kwenye kanzidata ya LATRA, ambapo kati yao, madereva 3,254 (sawa na asilimia 37.3) walijitokeza kufanya mitihani ambapo madereva 1,518 wamefaulu na kuthibitishwa na LATRA. Hivyo, madereva hao 1,518 ndio watakaotunukiwa vyeti vya kuthibitishwa na LATRA katika hafla hii.
Kwa hakika hii ni hatua kubwa kwetu. Madereva hawa watastahiki kupatiwa kitufe cha utambuzi (i-button) chenye taarifa za kila dereva husika. I-button ni mali ya dereva, sio mwajiri, na kinapaswa kutumika kila wapoanza safari na kumaliza safari. Nawashukuru sana madereva wetu na niwatie moyo wa kujiendeleza zaidi ili tupate hoja za kuweza kurasimisha ajira zao.
Aidha, naomba niwakumbushe na kuwafahamisha Watanzania kuwa madereva 999 tuliowathibitisha tarehe 1 Julai, 2023 na baadhi yao tuliowapatia i-button, walikuwa ni moja ya sababu kuu ya Serikali kukubali maombi ya wadau na kuruhusu safari za mabasi usiku (24/7). Sharti ambalo tumeweka wakati huo ni kwa mabasi yote yanayoomba ratiba za usiku ni lazima iwe na madereva waliothibitishwa na LATRA na kupatiwa i-button. Sasa, tumejifunza baadhi wanafanya udanganyifu, tutakwenda kuwafutia safari za usiku, lakini pia tunakoelekea ni kila basi kabla hatujatoa leseni na ratiba za usiku na hata mchana (24/7) lazima madereva wake watakaoendesha wawe wamethibitishwa na LATRA na watumie i-button.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Moja ya masharti ya leseni zinazotolewa na LATRA ni wenye vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara, kuhakikisha kila dereva anayeendesha vyombo hivyo ana Cheti cha Uthibitisho kinachotolewa na Mamlaka baada ya kufanya mtihani wa kuthibitishwa na kufaulu. Sharti la leseni kwa mtoa huduma za usafiri wa abiria kutumia dereva mwenye cheti cha uthibitisho kinachotolewa na Mamlaka, limeainishwa kwenye Kanuni ya 22(i) ya Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria), 2020. Madereva waliothibitishwa wanahimizwa kuzingatia Sheria na Kanuni za LATRA ili kuepuka kufanya makosa yatakayopelekea kufutiwa vyeti.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Zipo faida nyingi za madereva kuthibitishwa ikiwemo kurasimisha fani ya udereva ili iheshimike kama zilivyo fani zingine, kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazo wezesha kusimamia maslahi ya madereva katika ajira, kuwawezesha madereva kutambulika rasmi kikanda na kimataifa, kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa madereva pamoja na kuboresha uchunguzi wa matukio ya ajali pindi zinapotokea.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Nimalizie hotuba yangu kwa kuwakumbusha madereva wetu kuwa, Oktoba 01, 2023, Serikali ilitangaza kurejeshwa kwa safari za usiku (saa 24) ambazo zilikuwa ni kilio cha muda mrefu cha wasafirishaji, wamiliki na wananchi kwa jumla. Safari hizi zimekuwa na tija kwa kuwa zimeendelea kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii kwa watanzania. Hivyo, nawasihi madereva wote wanaoendesha mabasi yenye ratiba za usiku kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu. Halikadhari, nawasihi madereva ambao bado hawajasajiliwa, wahakikishe wanajisajili na kufanya mtihani ili kuthibitishwa na Mamlaka ili kujiongezea thamani katika kazi zenu na mkumbuke kuwa hili ni takwa la kisheria.
Aidha, naomba nitumie jukwaa hili kutoa maelekezo ya kiudhibiti kwa wamiliki wa vyombo vya moto na madereva wote walisajiliwa na kuthibitishwa na LATRA kisha kupatiwa vifaa vya utambuzi (i-buttons), wahakikishe wanatumia vifaa hivyo muda wote (24/7). Na kuanzia tarehe 1 Julai, 2024, hatutatoa leseni kwa basi ambalo halina dereva aliyethibitishwa na LATRA. Tumetoa muda wa kutosha, tuende kutekeleza Sheria sasa, tusikubali kuendeshwa na madereva wasioweza kufuatiliwa mwenendo wao, na wanaposababisha ajali wanakimbia. Milango ya kusikiliza mwenye tatizo ipo wazi ili asikwame kufanya biashara ya usafirishaji.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima naomba sasa nikukaribishe uongee na hadhara hii, kisha nakuomba utekeleze jukumu kubwa la kufungua kuwatunuku vyeti madereva 1,518 wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma ya usafiri kibiashara ambao wamefaulu mitihani na wamethibitishwa na LATRA.
Asanteni kwa kunisikiliza.
CPA Habibu J. Suluo
MKURUGENZI MKUU LATRA