Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA PROF. AHMED MOHAMED AME, MWENYEKITI WA BODI YA LATRA KATIKA HAFLA YA UTOAJI WA KADI KWA WAHUDUMU WA MABASI YA ABIRIA WALIOHITIMU MAFUNZO NA KUSAJILIWA NA LATRA
12 Nov, 2024 Pakua

Mheshimiwa David Kihenzile, Mbunge na Naibu Waziri wa Uchukuzi,

DCP Johansen Kahatano, Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu LATRA,

Ndugu Wawakilishi wa Taasisi za Mafunzo (CBE, NIT & ARUSHA TECH),

Wawakilishi wa Kituo cha Kuhifadhi Kumbukumbu Kimtandao (NIDC),

Wawakilishi wa Taasisi za Umma Mliopo,

Menejimenti na Wafanyakazi wa LATRA Mliopo hapa,

Ndugu Wanahabari, Wageni waalikwa, mabibi na mabwana,

 

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujaalia afya njema na fursa ya kujumuika hapa leo kwa lengo la kuandika historia mpya katika Nchi yetu ya kuwatambua rasmi wahudumu wa mabasi kwa kuwapatia kadi za utambulisho wa wahudumu wa vyombo vya usafiri ardhini waliotimiza vigezo. Inapendeza sana kuwaona wadau wetu mmefika hapa, hususan wale waliotupa sababu ya kukutana mahali hapa leo ambao ni wahudumu wa vyombo vya usafiri ardhini.

Aidha, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), natoa shukrani za dhati kwa viongozi wetu, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Waziri wa Uchukuzi, wewe Mhe. David Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Prof. Godius W. Kahyarara, Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi na Bw. Ludovick Nduhiye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi kwa kazi kubwa mnayoifanya katika Wizara yetu hususan katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa namna mnavyotuongoza vyema katika kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo. Tunatambua mnafanikiwa kutokana na uongozi madhubuti wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Kwa namna ya kipekee zaidi, niwashukuru sana Wakuu wa Vyuo (Chuo cha Elimu ya Biashara – CBE na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji – NIT) pamoja na wahadhiri wao kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kuandaa Mtaala wa kutoa mafunzo ya  Wahudumu wa Usafiri Ardhini. Baada ya uzinduzi wa mtaala uliofanyika tarehe 1 Julai, 2023, mwezi Novemba, 2023 Mamlaka ilifanya hafla ya uzinduzi wa mafunzo kwa wahudumu.  Hadi kufikia mwezi Oktoba, 2024 wahudumu 798 wamepata mafunzo ambapo katika wahudumu hao, NIT wametoa mafunzo kwa wahudumu 728 na CBE wahudumu 70. Katika wahudumu waliopata mafunzo katika vyuo hivyo, wahudumu 279 wamesajiliwa kwenye mfumo wa Mamlaka na wahudumu 174 wamekidhi vigezo na kutengenezewa kadi za utambulisho za LATRA na leo tumeandaa hafla hii fupi kwa ajili ya kuwakabidhi kadi wahudumu 174. Asanteni sana vyuo washirika kwa kazi kubwa mliyofanya na mnayoendelea kuifanya, na kipekee zaidi nawapongeza NIT kwa kutoa mafunzo kwa wahudumu wengi zaidi.

Pamoja na wahudumu kupata mafunzo kutoka vyuo hivyo, bado mwitikio wa usajili kwa ajili ya kupata kadi za uthibitisho uko chini sana, pamoja na jitihada zinazofanywa na Mamlaka za kuhamasisha wahudumu wote waliopata mafunzo kujisajili.  Ili kuongeza hamasa na mwitikio, Mamlaka inatoa kadi kwa wahudumu 100 leo waliothibitisha kushiriki uzinduzi huu.

Pia nawashukuru sana wadau wetu wote mliohudhuria hapa kwa kukubali mwaliko wetu na kujumuika nasi siku hii muhimu kushuhudia wahudumu wa vyombo vya usafiri kibiashara wakikabidhiwa kadi maalum za utambuzi.  Nafahamu kuwa mnayo majukumu mengi na makubwa yenye maslahi kwa Taifa, hata hivyo mmeweza kutenga muda wenu na kufika hapa ili kushuhudia jambo hili ambalo pia ni la maslahi makubwa kwa Watanzania na Taifa letu kwa jumla katika kuboresha huduma za usafiri ardhini.  Asanteni sana.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Naomba niwakumbushe kuwa LATRA inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kifungu cha (5)(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413. Miongoni mwa majukumu hayo ni kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa sekta zinazodhibitiwa.

Jukumu hili tulilopewa LATRA kwa mujibu wa Sheria, linalenga kuhakikisha kwamba, Watanzania wanapata huduma bora za usafiri ardhini zinazotolewa na wahudumu wenye weledi waliopata mafunzo sahihi yenye kuzingatia Sheria ya LATRA na Kanuni zake, Sheria ya Usalama Barabarani na Kanuni zake, huduma bora kwa wateja (abiria), jinsi ya kutoa huduma ya kwanza iwapo abiria atapatwa na changamoto zinazohitaji msaada huo, usalama wa watu na mali, na utunzaji wa mizigo

 

 Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Ili kutekeleza jukumu la Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva wa Vyombo vya Moto vinavyotoa Huduma za Usafiri Kibiashara kwa usafiri wa barabara na reli, Waziri mwenye dhamana ya Uchukuzi alitoa Kanuni  mbili (2) zifuatazo:

 

 

 Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Ili kutekeleza jukumu la Kusajili Wahudumu na Kuthibitisha Madereva wa Vyombo vya Moto vinavyotoa Huduma za Usafiri Kibiashara kwa usafiri wa barabara na reli, Waziri mwenye dhamana ya Uchukuzi alitoa Kanuni  mbili (2) zifuatazo:

  1. Kanuni za Uthibitishaji Madereva wa Magari ya Kibiashara na Usajili wa Wahudumu, yaani The Land Transport Regulatory Authority (Certification of Commercial Vehicle Drivers and Registration of Crew), Regulations, 2020, zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) Na. 81 la tarehe 7 Februari, 2020.  Hatua hii iliiwezesha Mamlaka kuanza kutekeleza jukumu la uthibitishaji wa Madereva ambapo leo hii tunatarajia kutoa kadi za utambulisho wa wahudumu.
  2. Kanuni za Uthibitishaji Madereva wa Treni na Usajili wa Wahudumu wa Treni, yaani The Land Transport Regulatory Authority (Certification of Train Drivers and Registration of Train Crew), Regulations, 2020, zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) Na. 80 la tarehe 7 Februari, 2020.  Hata hivyo, Kanuni hii haijaanza kutekelezwa, wataalamu wetu wa sekta ndogo ya reli bado wako kwenye maandalizi ya utaratibu utakaotumika.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Ninapenda nitumie nafasi hii kuwajulisha watoa huduma za usafiri nchini na wadau wote kwa ujumla kwamba kinachofanyika leo ni kutekeleza takwa la kisheria na kikanuni. Kwa mujibu wa kanuni ya 20(1)(d) ya Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili Wahudumu za mwaka 2020, kila mhudumu anayefanya kazi kwenye chombo cha usafiri kibiashara hususan magari ya abiria anatakiwa kuwa na Kadi ya Usajili iliyotolewa na Mamlaka.

Pamoja na takwa la kisheria na kikanuni, zifuatazo ni faida za wahudumu wetu kuhudhuria mafunzo na kusajiliwa na LATRA: 

  • Wamiliki kupata wasimamizi mahiri na wenye weledi wa kazi waliyopewa;
  • Wahudumu kufanya kazi kwa weledi, umakini na ufanisi zaidi;
  • Kuboresha huduma za usafiri ardhini;
  • Kurasmisha kazi ya wahudumu iheshimike kama zilivyo kazi nyingine;
  • Kulinda mitaji ya wamiliki wa vyombo na vipato vya wahudumu;
  • Kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowezesha kusimamia maslahi ya wahudumu katika ajira;  na
  • Kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa wahudumu na watumiaji wa huduma.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Kutokana na faida nyingi za wahudumu kusajiliwa, nihitimishe kwa kutoa wito kwa wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanawapatia wahudumu wao muda wa kuhudhuria mafunzo na hatimaye kusajiliwa. Muda wowote kuanzia sasa tutaanza kuchukua hatua dhidi ya wamiliki watakaotumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na kwa upande mwingine wahudumu ambao hawajasajiliwa hawataruhusiwa kutoa huduma kwenye mabasi. Hivyo, kila mdau ahakikishe anatakeleza matakwa ya sheria na kauni zilizopo katika utoaji wa huduma za usafirishaji abiria nchini.

 

Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Sasa napenda nitumie fursa hii kukukaribisha ili uongee na hadhara hii na hatimaye utekeleze kazi ya kihistoria ya kukabidhi kadi za utambulisho wa wahudumu wa mabasi.

 

Karibu sama Mheshimiwa Mgeni rasmi.

 

PROF. AHMED MOHAMED AME,

MWENYEKITI WA BODI YA LATRA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo