Ndugu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA);
Ndugu Wadau wa Sekta ya Uchukuzi;
Ndugu Wataalam kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na taasisi binafsi;
Waandishi wa Habari;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nawasalimu katika jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuturuzuku uhai na kutukutanisha leo, lakini kipekee niwashukuru washiriki wote kwa kutenga muda na kuja kujumuika nasi katika mkutano huu wa wadau wa Sekta ya Uchukuzi kwa lengo la kujadili na kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau juu ya Rasimu za Kanuni mpya tatu (3) za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini.
Ndugu Wadau,
Naamini mnafahamu kuwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeanzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Adhini, Sura 413 na kupewa jukumu la kudhibiti huduma za usafiri wa ardhini. Aidha, katika Sheria hiyo na Sheria ya Leseni za Usafirishaji, Sura 317, Waziri amepewa mamlaka ya kutengeneza Kanuni mbalimbali ili kuwezesha utekelezwaji wa Sheria hizi.
Ndugu Wadau,
Wakati LATRA inaendelea kutekeleza majukumu yake ya udhibiti, imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali zinazopelekea uhitaji wa kuwa na Kanuni hizi ili kutatua changamoto hizo. Miongoni mwa changamoto ni:
- kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi za kushughulikia utoaji, usitishwaji na ufutwaji wa leseni kwa watoa huduma kwa njia ya Reli;
- kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi zinazoainisha utaratibu wa kutoa vibali na leseni kwa ajili ya usimikaji na uendeshaji wa usafiri wa waya; na
- kutokuwepo kwa Kanuni mahsusi zinazotoa utaratibu kuhusiana na leseni maalumu kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri wa umma.
Ndugu Wadau,
Kutokana na changamoto hizo, na ili kuiwezesha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kutekeleza majukumu yake ya udhibiti usafiri ardhini ipasavyo, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini imeandaa rasimu za Kanuni mpya tatu (3) kama ifuatavyo:-
1. Kanuni za Leseni za Watoa Huduma kwa Njia ya Reli za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024;
Kanuni hizi zimelenga kuwadhibiti watoa huduma za usafiri watakaotumia miundombinu ya reli iliyojengwa na Serikali. Kanuni hizi zimeweka utaratibu wa kutoa, kuhuisha na kufuta vibali na leseni kwa watoa huduma za usafiri wa reli.
2. Kanuni za Usafiri wa Waya za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024;
Kanuni hizi zimelenga kutekeleza kifungu cha 5(1)(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura 413 kwa kuweka Kanuni zitakazosimamia utaratibu wa kutoa vibali na leseni kwa ajili ya udhibiti wa usafiri waya.
3. Kanuni za Leseni Maalum za Sheria ya Utoaji wa Leseni za Usafirishaji za mwaka 2024;
Kanuni hizi zimelenga kutekeleza kifungu cha 26 cha Sheria ya Leseni za Usafirishaji, Sura 317 kwa kuweka utaratibu wa kutoa, kuhuisha na kufuta leseni maalumu kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri wa umma.
Ndugu Wadau,
Baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha Rasimu za Kanuni hizo tatu (3) kwa ajili ya maoni yenu ikiwa ni sehemu muhimu katika mchakato wa kuandaa Kanuni hizi. Nichukue fursa hii kuwaomba muwe huru kujadili Kanuni hizi zinazopendekezwa na kutoa maoni yenu yatakayoboresha utekelezaji wa Kanuni hizo ili kuleta tija katika sekta ya usafirishaji ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu.
BAADA YA KUSEMA HAYO NAOMBA KUTAMKA KUWA KIKAO KIMEFUNGULIWA RASMI, NIWATAKIE KIKAO CHEMA NA CHENYE MAFANIKIO