Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, pamoja na mambo mengine, Mamlaka ina wajibu wa kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma zinazodhibitiwa. Katika kutekeleza sehemu ya wajibu huo, Mamlaka inaandaa tuzo za Wasafirishaji Bora na Salama kwa huduma za mabasi zilizotolewa kuanzia tarehe 01 Julai 2023 hadi 30 Juni 2024.
Tuzo hizo zitatolewa ili kuchochea matumizi ya mifumo ya utoaji wa huduma bora na salama ya usafirishaji wa abiria kwa ufanisi na ubunifu hususan katika matumizi ya teknolojia. Washindi watakabidhiwa Tuzo katika Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yatakayofanyika tarehe 26 hadi 30 Agosti 2024 Mkoani Dodoma.
Washindani wamegawanywa katika makundi matatu; (i) Wasafirishaji WAKUBWA (wenye mabasi zaidi ya 30), (ii) Wasafirishaji wa KATI (wenye mabasi 11 hadi 30) na Wasafirishaji WADOGO (wenye mabasi matatu hadi 10).