Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) inautaarifu umma kuwa imesitisha leseni za usafirishaji abiria kwa mabasi 27 kwa kipindi cha mwezi Machi, 2023. Uamuzi huu umefanywa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(b) ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 na Kanuni ya 27(1)(c) na (d) ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Magari ya Abiria) za Mwaka 2020.
Hatua hii ni kutokana na vitendo vya kuingilia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kusababisha mfumo kutotuma taarifa kabisa ama kutuma taarifa kwa kurukaruka (skipping). Hapa kuna baadhi ya mabasi ambayo baada ya wataalamu wa Mamlaka kufanya uchunguzi, waligundua betri za vifaa vya kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTDs) zimeharibiwa na mifumo yake ya umeme kubadilishwa. Kadhalika, kuna mabasi ambayo yamekutwa yakiwa na mfumo wenye swichi inayotumiwa na dereva kuzima na kuwasha kifaa hicho (VTD). Lakini kibaya na hatari Zaidi, yapo mabasi ambayo yamebadilishwa mfumo (software) na kutuma taarifa za uongo kwenye kituo chetu cha ufuatiliaji. Utaona basi linasafiri mpaka linafisha kwa spidi isiyobadilika. Hapa, ni muhimu wamiliki wa mabasi na madereva wafahamu kuwa mfumo wa VTS una uwezo wa kutoa taarifa kwa Mamlaka iwapo utaingiliwa au kuharibiwa.