CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewaasa abiria wanaosafiri kwa mabasi yaendayo mikoani kuhakiki tiketi zao za safari kupitia Mfumo Jumuishi wa Utoaji Tiketi (CeTS) unaojulikana kwa jina la Safari Tiketi unaopatikana kwa anwani ya https://tiketi.latra.go.tz/ ili kuepuka ulanguzi wa tiketi unaosababisha kutozwa nauli isiyokuwa elekezi.
CPA, Dkt. Suluo amebainisha hayo Desemba 23, 2025 wakati akifanya kaguzi za usafiri wa mbasi yaendayo mikoani katika vituo mbalimbali vya mabasi mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2025.
“Tunawasisitiza abiria wote wanaosafiri hasa kipindi hiki za sikuku za mwisho wa mwaka na siku zote kuhakikisha taarifa zao za muhimu ikiwemo majina mawili au matatu yanakuwepo kwenye tiketi zao za safari kama ilivyo katika Kitambulisho Cha Taifa (NIDA) ili isaidie inapotokea dharura kujua nani alikuwa katika basi, kutokuwepo kwa taarifa hizo inasababisha ulanguzi wa tiketi,” amesema CPA, Dkt. Suluo.
Ameongeza kuwa, Mfumo wa Safari Tiketi unawezesha kumtambua abiria anayesafiri, kupata taarifa sahihi za abiria aliyekuwa safarini, kusuluhisha migogoro kwa abiria wawili wanaokatiwa tiketi moja kwa kuhakiki tiketi kupitia mfumo na abiria anaweza akahakiki tiketi yake mwenyewe ya basi lolote alilopenda kusafiri nalo
Vilevile amesema, mbali na hali ya usafiri kuwa ni nzuri kutokana na abiria kusafiri bila msongamano, zipo baadhi ya changamoto zimebainika katika vituo vya mabasi kwa baadhi ya wasafirishaji.
“Changamoto zilizobainika katika ukatajai tiketi kwa baadhi ya abiria ni majina yao kutokuwepo kwenye Mfumo na wao kukabidhiwa tiketi ambazo zina jina tofauti na majina yao kuandikwa kwa kutumia kalamu ya mkono kwenye tiketi ileile yenye jina lingine lakini ukihakiki tiketi hiyo kwenye Mfumo pia unakuta ina jina lingine hali inayosababisha tiketi moja kuwa na majina matatu tofauti,” ameeleza CPA, Dkt. Suluo.
Wakati huohuo CPA, Dkt. Suluo ameeleza kuwa takwimu ya abiria waliosafiri Desemba 23, 2025 kuwa ni jumla ya abiria 120,279 na jumla ya abiria 2,198,076 wamesafiri katika kipindi chote cha sikukuu za mwisho wa mwaka na miamala yote ya jumla imefikia bilioni 79 na miamala iliyofanyika Desemba 23, 2025 ni billion 4 ambayo malipo yake yaliyofanyika mtandaoni uwiano ni uleule wa shilingi 449,000,000 sawa na asilimia 11.
Mfumo wa Safari Tiketi ni Mfumo uliounganishwa na mifumo mingine ya utoaji tiketi ukiwemo wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na mifumo ya tiketi za mabasi unaomwezesha abiria kufanya wekesho la safari kwa kampuni ya mabasi anayoitaka, kukata tiketi kimtandao na kufahamu basi analotaka kusafiri nalo liko sehemu gani kupitia Mfumo wa Taarifa kwa abiria (PIS).

