Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

BODI YA WAKURUGENZI LATRA YATEMBELEA MRADI WA SGR
Imewekwa: 30 Apr, 2023
BODI YA WAKURUGENZI LATRA YATEMBELEA MRADI WA SGR

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imefanya ziara katika mradi wa maendeleo ya Reli ya Kisasa (SGR) kipande kinachoanzia Dar es salaam mpaka Morogoro.

Katika ziara hiyo, Bodi ya Wakurugenzi imetembelea sehemu mbalimbali za mradi huo ikiwemo chumba maalum chenye mitambo ya kuongoza safari za treni zinazopita katika kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutupora pia imetembelea njia inayopita treni kuanzia stesheni ya Reli ya Kisasa katika jengo la Tanzanite.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Ahmed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA amesema mradi wa SGR umepiga hatua kubwa na imeongeza hali ya usalama pindi itakapoanza kutumika.

“Maendeleo ya SGR yamepiga hatua kubwa sana na kufikia mahala pazuri ikiwemo kuwepo kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA inayoongoza safari za treni popote pale inapopita, mfumo huu utasaidia na kuimarisha usalama katika njia za treni ya kisasa kwa kuonesha makosa ya kibinadamu,” amesema Prof. Ame.

Naye Bw. Senzige Kisenge, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) amesema TRC imejikita katika kuboresha utendaji kazi wa reli ya kisasa kwa kutoa mafunzo jinsi ya kuongoza mifumo iliyowekwa kwa ajili ya kuongoza safari za reli.

“Yapo mafunzo yanayoendelea kutolewa hapa Dar es salaam ambayo yanayotolewa na mkandarasi aliyejenga mifumo hiyo ya kuongoza safari za treni ikiwemo mifumo inayohusu umeme na mawasiliano, mafunzo mengine yanaendelea kufanyika nchini Korea kwa kuwapeleka watu kupatiwa mafunzo ya jinsi ya kuendesha mifumo hiyo,” ameeleza Bw. Kisenge.

Uwepo wa Reli ya Kisasa na kuanza kufanya kazi itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa muda na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, mwananchi anaweza kutumia muda mfupi zaidi kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hivyo inaokoa muda ambao angeutumia kwa safari, kwa mfano safari ya Morogoro hadi Dar es Salaam ingemlazimu mwananchi kutumia hadi saa nne kwa gari lakini atatumia saa moja tu kwa treni ya SGR.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo