Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA, DKT. SULUO AWASIHI WATUMISHI WA LATRA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA KUJITUMA
Imewekwa: 16 Jan, 2026
CPA, DKT. SULUO AWASIHI WATUMISHI WA LATRA KUFANYA KAZI KWA BIDII NA KUJITUMA

CPA, Dkt. Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi watumishi wa LATRA kufanya kazi kwa moyo, bidii na kujituma huku wakizingatia Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (QMS) ISO 9001 ili kuacha tabasamu kwa wateja.

CPA, Dkt. Suluo amebainisha hayo Januari 16, 2026 katika Kikao cha Saba cha Baraza la Wafanyakazi la LATRA linachofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Magadu ,Mkoani Morogoro

“Tumepata ithibati ya Kimataifa ya kutoa huduma kwa viwango vya kimataifa hivyo tuendelee kutoa huduma bora kwa wateja tunaowahudumia. Tuendelee kushikamana  tukitambua kuwa tupo kwenye nafasi zetu kumsaidia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu  kutafakari tunachokifanya ili kuleta nyuso za tabasamu kwa wananchi,” amesema  CPA, Dkt. Suluo.

Vilevile amesema kuwa, anajivunia kuwa na watumishi wanaofanya kazi kwa juhudi na mafanikio ya LATRA yaliyopatikana ni matokeo ya utendaji mzuri wa watumishi hao.

Naye Bw. Mussa Mwakalinga, mwakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania –COTWU (T) amempongeza CPA, Dkt. Suluo, mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi LATRA kwa kuboresha Baraza hilo na kuendesha vikao hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Kikao hicho kinafanyika kwa siku mbili Januari 16 na 17, 2026 ambapo wajumbe wa Baraza hilo wamepatiwa mafunzo ya siku moja kuhusu Afya ya Moyo, Sheria ya Mirathi, Haki za Watoto pamoja na Sheria ya Ndoa.

Kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Baraza hilo wamepongeza mada zilizowasilishwa na wataalamu na wamesema elimu waliyopatiwa inaendana na mahitaji halisi yaliyopo.

Baraza la Wafanyakazi la LATRA linaendesha vikao vyake mara moja kwa mwaka na linajumuisha Wajumbe wa Menejimenti, Wawakilishi wa Watumishi wa Idara na Vitengo, Maofisa Wafawidhi wa Mikoa yote pamoja na Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania –COTWU (T)- Tawi la LATRA

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo