
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeshiriki mapokezi ya safari ya kwanza ya Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) iliyoanza safari rasmi kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo aliagiza safari hiyo kuanza rasmi Julai 25, 2024.
Akizungumza kutokea stesheni ya SGR Dodoma, CPA Habibu Suluo Mkurugenzi Mkuu LATRA ameipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa juhudi na usimamizi mkubwa wakukamilisha mradi huu na kuanza rasmi safari ya kwanza Dar es Salaam hadi Dodoma chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) Waziri wa Uchukuzi kwa kufanikisha jambo hili la kihistoria hapa nchini.
Vilevile CPA Suluo ameeleza kuwa, LATRA inajukumu la kudhibiti miundombinu ya Reli pamoja na kuhakikisha kuwa usafiri huu unakuwa rafiki na salama kwa kuboresha sehemu zenye mapungufu ili Wananchi waweze kusafiri salama na kwa wepesi.
“Maafisa wa LATRA wanaendelea kukagua njia ya Dar es Salaam hadi Dodoma ili kuboresha yale mapungufu machache yaliyobainika na kuhakikisha miundombinu inakuwa salama na rafiki kwa kila Mtanzania na kuwarahisishia wananchi kufika kwa wepesi, na niwasihi mtunze miundombinu hii bila kuiharibu,” ameeleza CPA Suluo.
Aidha ameeleza kuwa, LATRA imepanga nauli za SGR kwa watu wazima na watoto kuanzia umri wa miaka minne hadi 12 ambazo ni nafuu kwa kila Mtanzania.
“Ni jukumu letu kupanga nauli za usafiri huu na kwa daraja la kawaida tumewazingatia Wananchi wa kawaida kwani watazimudu nauli hizi ambapo kwa treni itakayokuwa inasimama kila kituo ni shilingi 13,000 kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na shilingi 31,000 kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ambapo watoto chini ya miaka minne hawatalipia gharama hizo na watoto wenye umri wa miaka minne hadi 12 watalipia nusu gharama ya nauli hizo na nauli hizi zipo katika tovuti yetu www.latra.go.tz ’’ ameeleza CPA Suluo
Ameongeza kuwa “Treni hii iliyokuja leo ni ya haraka yaani (express), hii nayo ina nauli yake na inasimama vituo viwili tu yanii Morogoro na Dodoma na nauli yake ni Shilingi 22,000 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, na shilingi 50,000 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma lakini TRC wanatoza 40,000 na hawatakiwi kushusha zaidi ya hapo,’ aliongeza.
LATRA inaendelea kushirikiana na wadau wengine wa usafiri ili kuhakikisha huduma bora na salama kwa wananchi wote. Uzinduzi wa safari hii mpya ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha sekta ya usafiri na kuunganisha miji mikubwa nchini.