
CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi wadau wa sekta ya usafiri ardhini wakiwemo wasafirishaji, watoa huduma na watanzania wote kuungana pamoja kuilinda, kuitunza na kuienzi amani ya nchi na pia amewasihi wanahabari kutoa habari zinazowaleta watanzania pamoja na zinazolenga kudumisha amani.
CPA Suluo amebainisha hayo Oktoba 08, 2025 ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika Oktoba 06 hadi 10, 2025 yenye kaulimbiu “Mission: Possible” yaani Mipango Imewezakana.
“Tunawashukuru wadau wetu kwa kuwa nasi bega kwa bega katika kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji nchini na tunafurahi tunasherehekea pamoja wiki hii ya huduma kwa wateja tukiwa na amani na utulivu. Niwakumbushe kuwa nchi yetu inaelekea kwenye kipindi cha uchaguzi mkuu, nawasihi tuenzi amani ya nchi yetu, tudumishe umoja na mshikamano wetu kama watanzania na tarehe 29 tujitokeze kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura tulivyojiandikisha ili tukatumie haki yetu ya kikatiba kwa kupiga kura kwa amani,” amesisitiza CPA Suluo.
Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, CPA Suluo alishiriki kikamilifu kutoa huduma, kusikiliza maoni na kutatua changamoto za wateja waliotembelea ofisi ya LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.