Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

CPA SULUO: HAKIKISHENI MNAPATIWA TIKETI ZA KIELEKTRONI ZENYE TAARIFA ZENU SAHIHI
Imewekwa: 21 Dec, 2024
CPA SULUO: HAKIKISHENI MNAPATIWA TIKETI ZA KIELEKTRONI ZENYE TAARIFA ZENU SAHIHI

CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewaasa abiria kuhakikisha wanapatiwa tiketi za kielektroni zenye taarifa zao sahihi pindi wanaposafiri na mabasi ya masafa marefu kwa kuwa Mfumo wa tiketi unaotumika umeunganishwa na LATRA pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hivyo itarahisisha ufuatiliaji wa bima kwa ajili ya kuwafidia abiria endapo itatokea dharura safarini.

CPA Suluo amebainisha hayo baada ya ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, kituo cha mabasi Magufuli Dar es Salaam Desemba 21, 2024, kwa lengo kuangalia hali ya usafiri na kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka 2024.

Aidha amesema, ukaguzi huo umeangazia utekelezaji wa masharti ya leseni ikiwemo matumizi sahihi ya Kitufe cha Utambuzi wa Dereva (i- Button), matumizi sahihi ya Tiketi mtandao pamoja na Jeshi la Polisi kupima kiwango cha ulevi kwa madereva wa mabasi ya masafa marefu.

“Ni jukumu letu kuhakikisha mabasi yapo na abiria wanasafiri kwa nauli ambayo tumeipanga, na tumebaini kuwa hali ni nzuri na abiria wote wamesafiri usiku na asubuhi ya leo tumekagua nakuona tiketi zimetolewa lakini kunatatizo dogo kwa wale abiria ambao wanashuka njiani mfano abiria wanaopanda magari yanayoenda Musoma na kushuka Morogoro hawapewi tiketi na hii ni hatari kwa usalama wao,”amesema CPA Suluo.

Vilevile amewasihi abiria kutumia Mfumo wa PIS unaopatikana kwa anwani ya https://pis.latra.go.tz/ ili kufahamu mwendokasi wa basi na endapo watabaini mwendo hatarishi wa dereva, wapige simu bila malipo kwa LATRA kupitia namba 0800110019 au 0800110020 saa 24 siku zote.

Ameongeza kuwa, LATRA inatumia Mfumo wa kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kufuatilia kwa ukaribu mabasi yote na kupitia i-Botton wanaona mwenendo mzima wa dereva na hivyo amewasihi madereva kuendesha mabasi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Wakati huohuo, CPA Suluo amesema kuwa, wasafirishaji wenye mahitaji ya ziada wawasilishe maombi kwa Mamlaka kwa magari ambayo yana siti zaidi ya 40 ili kupatiwa vibali vya muda, muhimu msafirishaji awe amekidhi masharti ya leseni ikiwemo kufunga Mfumo wa VTS, awe na mfumo wa kutolea tiketi na dereva anayesafiri awe amethibitishwa na Mamlaka.

“Hadi sasa Mamlaka imetoa vibali vitatu tu kwa mkoa wa Arusha na Manispaa ya Moshi na hali hii ni matokeo mazuri ya safari za saa 24 ambapo kwa sasa hali ya usafiri imekuwa ni salama na hakuna msongamano wa abiria katika vituo vya mabasi,” ameeleza CPA Suluo.

Akizungumzia udhibiti wa huduma za usafiri wa treni Nchini CPA Suluo amesema kuwa, wataalamu wa LATRA wanaendelea na kazi ya ukaguzi wa miundombinu na pia safari za Reli ya Kisasa (SGR) zinazofanya safari za Dar es Salaam hadi Dodoma na reli ya kati inayofanya safari za Dar es Salaam hadi Arusha kwa sasa imeongezwa safari za mara tatu kwa juma ambazo zimepunguza msongamano wa abiria.

Naye DCP Ramadhani Nga’nzi, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kufanya ukaguzi barabarani katika vituo mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali zao.

“ Leo tumefanya ukaguzi wa kawaida kwa kushirikiana na LATRA  pamoja na kutoa elimu kwa madereva kuwa, watimize wajibu wao na pia tumepima kiwango cha ulevi kwa madereva na ukaguzi huu unaendelea nchi nzima na tutahakikisha abiria wote wanakuwa salama. Tunaamini Tanzania bila ajali inaezekana na tunawaasa madereva wote wa malori, magari na bodaboda wazingatie Sheria za usalama barabarani na watupe ushirikiano, na wale watakaokikuka Sheria, hatutosita kuwachukulia hatua kali za Kisheria,” amesema DCP Nga’nzi.

Kwa upande wake Bw. Daudi Daudi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC), ametoa rai kwa abiria kutimiza wajibu wao na pia kupata haki zao za msingi ikiwemo kupewa tiketi za kielektroni na kupata muda wa dakika 20 za huduma za kijamii wanapokuwa safarini.

LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani inaendelea na ukaguzi nchini katika vituo mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali zao katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka 2024 na mwanzo wa mwaka 2025.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo