
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imewasihi watoa huduma za usafiri wa magari ya abiria ya masafa marefu kuwahimiza wahudumu waliowaajiri kupata mafunzo kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) au Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), na tarehe 31 Disemba, 2024 ndio mwisho kwa wasafirishaji kutumia wahudumu ambao hawajasajiliwa na LATRA.
Hayo yamebainishwa na Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano - LATRA alipozungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano ofisi za LATRA Dar es Salaam Agosti 14, 2024.
Aidha, Bw. Pazzy ameongeza kuwa, baada ya mafunzo, wahudumu hao watatakiwa kuwasilisha maombi ya kusajiliwa LATRA kwa mujibu wa taratibu zilizopo kupitia Mfumo wa Maombi ya Leseni za Usafirishaji (RRIMS) unaopatikana kwa anwani ya https://rrims.latra.go.tz/login ili kupatiwa kadi ya usajili ya mhudumu kwa mabasi ya abiria,
“Mamlaka inawakumbusha wahudumu wote ambao wamepata mafunzo, kutuma maombi ya kusajiliwa kupitia https://rrims.latra.go.tz/login kwa kutumia Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au kufika ofisi yoyote ya LATRA. Maombi yaambatishwe na Cheti cha mafunzo na picha mbili za pasipoti zenye kivuli cheupe,” amesisitiza Bw. Pazzy.
Vilevile, Bw. Pazzy amezitaja faida za wahudumu kusajiliwa na LATRA kuwa itasaidia kurasimisha fani na ajira zao, kuongeza uwajibikaji katika kutoa huduma kwa mujibu wa Sheria pamoja na kujenga ari ya umoja na mshkamano wa wahudumu hao katika masuala ya haki na wajibu wao .
Kwa upande wake Dkt. Nasibu Mramba, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo - CBE ameeleza kuwa, uongozi wa CBE unashirikiana na LATRA na wadau wengine kuwapatia mafunzo wahudumu wa mabasi ya masafa marefu kwenye maeneo ya Kanuni, Sheria na maadili ya usafirishaji wa abiria pamoja na usalama ili kuhakikisha abiria wanapatiwa huduma bora.
Naye Bi. Honesta Mjaki, Mratibu wa Mafunzo ya Watoa Huduma - NIT, ameeleza kuwa, Chuo cha NIT kimetoa mafunzo kwa wahudumu 503 na kimewafikia wahudumu wa kampuni mbalimbali Tanzania Bara na amewasihi wahudumu kujitokeza kwa wingi kupatiwa mafunzo.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, Mamlaka ina jukumu la kusajili wahudumu na kuthibitisha madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara. Pia, Kanuni ya 17 ya Kanuni za Uthibitishaji Madereva na Usajili Wahudumu wa Magari ya Biashara za Mamlaka ya Udhibiti usafiri Ardhini (LATRA) za mwaka 2020, zinamtaka mtu yeyote anayekusudia kufanya kazi ya uhudumu katika gari linalotoa huduma za usafiri kibiashara kusajiliwa na LATRA.