Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KAMATI YAIPONGEZA LATRA TIKETI MTANDAO
Imewekwa: 25 Aug, 2023
KAMATI YAIPONGEZA LATRA TIKETI MTANDAO

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Miraji Mtaturu (Mb) ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kusimamia Mfumo wa Tiketi Mtandao kwani umepunguza kero kwa abiria wa usafiri wa ardhini nchini.

Akizungumza jijini Dodoma wakati Kamati hiyo ikipokea taarifa ya Utendaji ya Mamlaka hiyo Mhe. Mtaturu amesema miongoni mwa faida za mfumo huo ni pamoja na kupunguza mianya ya uvujaji wa mapato kwani abiria ana uhuru wa kukata tiketi na hali hiyo kuruhusu mmiliki kuona idadi ya siti zilizokatwa.

“Nawapongeza sana LATRA sababu kupitia mfumo wa tiketi mtandao sasa hivi abiria anaweza kukata tiketi akiwa popote bila kulanguliwa na maajenti, lakini mfumo huu umerahisisha ukusanyaji wa mapato kwa wamiliki na Serikali sababu unaweza kuona idadi za tiketi moja kwa moja kupitia mfumo’’ amesema Mhe. Mtaturu.

Aidha, Mhe. Mtaturu ameitaka LATRA kuhakikisha Kampuni ya Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) zinaharakisha kuingia kwenye mfumo wa   tiketi mtandao ili kuwarahisishia abiria kwani wamekuwa wakitumia muda mrefu kupanga mistari katika stesheni ili kupata tiketi.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta a Ujenzi), Mhe. Atupele Mwakibete amesema Serikali imeanza kutekeleza mkakati madhubuti wa kudhibiti ajali kwa kufanya utafiti kupitia gari maalum likalobainisha maeneo yenye changamoto za ajali ili kuja na suluhu itakayosaidia kuondoa ajali zinazosababishwa na ubovu wa barabara.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa LATRA CPA Habib Suluo ameihakikishia Kamati kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu na kufanyia kazi ushauri uliotolewa kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha abiria wanasafiri kwa usalama.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo