
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetoa siku 14 kuanzia Julai 2, 2025 kwa Kampuni sita (06) za Tiketi Mtandao ambazo bado mifumo yao ina changamoto na imezitaka kuzitatua ili kuidhinishwa na watakaoshindwa hawataruhusiwa kuendelea kutoa huduma hiyo.
Amebainisha hayo Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano LATRA alipoongea na vyombo vya habari ukumbi wa mikutano ofisi za LATRA Dar es Salaam Julai 2, 2025.
Bw. Pazzy amezitaja kampuni hizo kuwa ni AB Courier Express Limited, Busbora Company Limited, Logix Company Limited, Mkombozi Infotech Company, Sepatech Company Limited na Web Corporation Limited.
Vilevile Bw. Pazzy ameeleza kuwa, kampuni tatu (03) zimekidhi vigezo na zinaendelea kukamilisha taratibu zingine ili waweze kupatiwa kibali cha utoaji huduma za Tiketi Mtandao.
“Hadi tarehe 30 Juni, 2025, kampuni ya Otapp Agency Company Limited, Hashtech Tanzania Limited na Iyishe Company Limited zimekidhi vigezo vya kupata kibali cha kutoa huduma za Tiketi Mtandao kwa mujibu wa Sheria na Mamlaka imeruhusu kampuni hizo kufanya malipo ili kukabidhiwa vibali vyao,” amefafanua Bw. Pazzy.
Aidha ameeleza kuwa, kampuni ya Duarani Innovative Company na Itule Company zimebainika kuwa na changamoto na kukosa sifa za kutoa huduma ya Tiketi Mtandao na hivyo wamepewa siku (07) za matazamio na wakishindwa hawataruhusiwa kutoa huduma na wateja wao watashauriwa kuhamia kwa watoa huduma waliokamilisha utaratibu.
Vilevile amesema, watoa huduma wote wanapaswa kukamilisha na kuendelea kutekeleza matakwa ya kisheria ya kuunganisha mifumo yao na mfumo mkuu wa Tiketi Mtandao (CeTS) ikiwa ni pamoja na kuingiza taarifa za mabasi yote wanayoyahudumia kwenye Mfumo Jumuishi wa Tiketi Mtandao wa Mamlaka (UTS) na watoa huduma wote ambao hawapo katika orodha iliyotajwa hawatambuliki na Mamlaka kwa mujibu wa Sheria.
Kanuni ya 5 ya Kanuni za Tiketi Mtandao za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2024 zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 20 la Januari 12, 2024 zimeweka vigezo vya kupata kibali ambavyo ni pamoja na mfumo husika kuwa na ulinzi dhidi ya uvamizi wa kimtandao na kuwa na uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya Serikali.