Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

KASAGARA: WASAFIRISHAJI JIUNGENI KWENYE MFUMO WA TIKETI MTANDAO
Imewekwa: 08 Feb, 2023
KASAGARA: WASAFIRISHAJI JIUNGENI KWENYE MFUMO WA TIKETI MTANDAO

Na Mambwana Jumbe

Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Mkoani Mwanza Bw. Emil Kasagara amewataka wasafirishaji wa mabasi ya masafa marefu kujiunga na kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao na kuunganisha mifumo yao kwenye Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Risiti za Kielektroni (EFDMS) ili mifumo hiyo iweze kubadilishana taarifa.

Kasagara amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Mhe. Adam Malima kwenye semina kwa wananachama wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Mwanza Februari 8, 2023.

Bw. Kasagara amesema kuwa, Mfumo wa Tiketi Mtandao unaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za uendeshaji wa Sekta ya usafirishaji nchini pamoja na kufanya maamuzi mbalimbali kwa usahihi na pia unasaidia kupunguza upotevu wa mapato kwa wamiliki kwa kuwa wanapata fedha zao pindi abiria anapokata tiketi yake.

“Mfumo huu ni mahususi kwa ajili ya usafiri wa abiria, unaruhusu mtu yeyote kukata tiketi bila ya kwenda stendi au kwenye ofisi ya basi husika, hii ni faida kwa wasafiri maana inaokoa muda na inawasaidia kupunguza adha wakati wa ukataji wa tiketI,” ameeleza.

Aidha, amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha utendaji wake kwa njia ya mifumo ambayo imeongeza tija na maendeleo ya nchi kwa jumla.

Naye Meneja Mradi wa Tiketi Mtandao LATRA CPA Tadei Mwita amewasihi wasafirishaji kuzingatia Kanuni za Leseni za Usafirishaji - Mabasi ya Abiria za mwaka 2020 kwa kuwa ndizo zinazowaongoza katika utoaji wa huduma za usafirishaji nchini.

Kanuni ya 22(j) inamtaka mwenye leseni ya kusafirisha abiria kutoa tiketi kwa kutumia mfumo wa tiketi wa Kielektroni ulioidhinishwa na LATRA na Kanuni ya 23(b) na 24(d) inamtaka mwenye leseni ya kusafirisha abiria ahakikishe tiketi ya kielektroni inatolewa kwa kila abiria,” ameeleza CPA Mwita.

Ameongeza kuwa, Kanuni ya 30 inamtaka mtoa huduma ya usafiri wa abiria kutotoza nauli inayozidi kiwango kilichoidhinishwa kwa daraja husika la gari na Kanuni ya 32(1)(b) Mtoa huduma ya usafiri wa abiria ahakikishe wafanyakazi wa ndani ya gari wanapewa vifaa vya kuwawezesha kutoa tiketi za kielektroni.

Akizungumzia taarifa muhimu zinazotakiwa kuwekwa kwenye tiketi ya kielektroni, CPA Mwita amesema Kanuni ya 32(2)(a) inaelekeza tiketi iwe na Jina la abiria na namba ya siti, Muda wa abiria kufika na muda wa kuanza safari na Kituo cha kuanzia safari, njia itakayotumika na kituo cha mwisho cha safari. Vilevile Kanuni ya 32(2)(a) Tiketi iwe na Nauli ya safari, Anwani na namba za simu za mtoa huduma, Namba ya gari, Tarehe ya tiketi kutolewa na tarehe ya safari pamoja na Namba ya  tiketi (Serial number).

Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja TRA Mkoa wa Mwanza Bi. Millicent Igogo amesema TRA na LATRA wataendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa wasafirishaji wanapata elimu na wanatumia Mfumo wa Tiketi Mtandao kwa kuwa umekuwa na tija kwa Serikali, Wamiliki na Wananchi kwa jumla

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo