Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA, DCEA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI USAFIRISHAJI WA DAWA ZA KULEVYA
Imewekwa: 12 Jul, 2025
LATRA, DCEA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI USAFIRISHAJI WA DAWA ZA KULEVYA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) zimepanga kushirikiana kutoa elimu ya namna bora ya kudhibiti vitendo vya usafirishaji wa dawa za kulevya kwa wamiliki wa mabasi ya masafa marefu, madereva na wahudumu (makondakta) ambao wamekuwa wakishiriki kwa kujua ama kutokujua kusafirisha dawa hizo kwenye mabasi.

Akizungumza alipotembelea jengo la LATRA kwenye maonesho ya 49 ya biashara ya kimataifa (Sabasaba) Bw. Aretas James Lyimo, Kamishna Jenerali DCEA amesema elimu hiyo inahusu Sheria ya kudhibiti dawa za kulevya na Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini ili kuwaeleza kuhusu athari za kujihusisha na vitendo vya usafirishaji wa dawa za kulevya kwenye vyombo vya moto kibiashara.

“Tunatoa elimu kwa madereva, makondakta na wamiliki wa magari ili waelewe kwamba wanapokamatwa na dawa za kulevya kupitia basi au chombo cha moto anachoendesha, dereva na kondakta wanahusika moja kwa moja kwa kuwa wao wamepakia mzigo na ndio wenye dhamana na basi likiwa safarini hivyo wanapaswa kuelewa aina ya mzigo waliopakia kwenye basi lao,” ameeleza Bw. Lyimo.

Bw. Lyimo ameongeza kuwa, wamiliki wa mabasi wamekuwa wakilalamika pindi magari yao yanapokamatwa na dawa za kulevya hivyo kupitia elimu wataelewa kuwa basi nalo linahusika kwa kuwa ndio limebeba dawa hizo na ni kielelezo namba moja mahakamani

“Nawasihi wamiliki wa vyombo vinavyodhibitiwa na LATRA kuajiri madereva na wahudumu wenye uadilifu na wahakikishe wanaingia nao mkataba wa kukataza kubeba dawa za kulevya kwenye chombo kwa kuwa itakapobainika, wote watakuwa na hatia ya kusafirisha dawa hizo ambapo msafirishaji atapata kifungo cha maisha kutokana na kile alichokibeba au kifungo cha miaka 30 jela na chombo kilichobeba nacho kitataifishwa,” amesema Bw. Lyimo.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amewataka madereva na wahudumu wa vyombo vinavyodhibitiwa na LATRA kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria za nchi kwakuwa zimewekwa kwa ajili ya kulinda jamii.

Vilevile amesema LATRA inatoa leseni za usafirishaji zenye masharti yanayopaswa kuzingatiwa na msafirishaji ikiwemo vitu vinavyopaswa kusafirishwa, pia Sheria na Kanuni za Mamlaka zinaelekeza mhudumu kukagua mzigo kabla hajaweka alama

 CPA Suluo vilevile amewasihi wasafirishaji kuajiri madereva waliothibitishwa na wahudumu waliosjiliwa na LATRA lakini pia wahakikishe wanakuwa na utamaduni wa kufanya kazi kwa maadili ikiwemo kukataza kubeba dawa za kulevya.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo