
Bi. Happiness Sulle, Katibu Tawala Wilaya ya Mkalama - Singida ameiasa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa waliopo vijijini ili kuwaongezea uelewa wa majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na LATRA.
Bi. Sulle amebainisha hayo alipotembelea banda la LATRA lililopo Viwanja vya Nzuguni, Dodoma kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika kuanzia Agosti 1 hadi 10, 2025 ambapo alielezwa majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na LATRA katika sekta ya usafiri ardhini nchini.
“Nawasihi kuendelea kutoa elimu hadi ngazi za vijijini ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, ili wafahamu kazi, majukumu yenu na hatimaye waweze kutumia vizuri huduma za usafiri ardhini. Pia mnapaswa kuongeza ubunifu ili kuendana na teknolojia ya sasa katika utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema Bi. Sulle.
Vilevile ameipongeza LATRA kwa jitihada za kuboresha sekta ya usafiri ardhini zinazochagiza mapinduzi katika usimamizi wa huduma za usafiri nchini hasa kupitia mifumo ya kidigitali.
Kwa upande wake Bw. Ezekiel Emmanuely, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Dodoma amesema, “LATRA inatambua umuhimu wa kuwafikia wananchi kwa kutoa elimu ya moja kwa moja, maonesho haya ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kufikia wananchi kwa kuwaelimisha kuhusu haki, wajibu na huduma bora za usafiri ardhini.”
Naye Mha. Dkt. Prosper Mgaya, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ametembelea banda la LATRA na amejifunza kuhusu Mifumo inayotumiwa na LATRA katika shughuli za udhibiti na ameeleza namna NIT inavyoshirikiana na LATRA katika kuboresha sekta ya usafiri nchini.
“Ushirikiano kati ya NIT na LATRA unaendelea kuleta manufaa makubwa katika sekta ya usafiri hasa kwa kutoa wataalamu waliobobea katika usimamizi na udhibiti wa usafiri ardhini na leo nimejifunza Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) ambao unamrahisishia abiria kupata taarifa mbalimbali za mabasi yanayowasili katika vituo vya mabasi pamoja na kutambua mwenendo wa basi linapokuwa safarini, hii inadhihirisha ubunifu wenu mkubwa kupitia mifumo ya kidijiti,” amesema Mha. Dkt. Mgaya.
LATRA inashiriki katika maonesho haya kwa kuonesha mchango wa sekta ya usafirishaji katika kufanikisha maendeleo ya kilimo na biashara nchini, kupitia udhibiti bora wa usafiri wa mazao, pembejeo na watu vijijini na mijini.