Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA Yaendesha Mkutano wa Wadau Kutathmini Mfumo wa Tiketi Mtandao
Imewekwa: 21 Jul, 2022
LATRA Yaendesha Mkutano wa Wadau Kutathmini Mfumo wa Tiketi Mtandao

Na. Mambwana Jumbe

Mara baada ya mfumo wa Tiketi Mtandao kuanza kufanya kazi rasmi Julai 1, 2022, leo Julai 21, 2022 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imefanya mkutano na wadau wa usafirishaji kutathmini utekelezaji wa mfumo huo na kujadili changamoto zinazojitokeza ili kuzifanyia kazi.

 

Mkutano huo umejumuisha wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu Kimtandao (NIDC) pamoja na watoa huduma za mifumo ya utoaji tiketi kimtandao.

 

Akiongea katika mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu J. Suluo amesema mkutano huo umeazimia kuwa tiketi zote za mabasi ya masafa marefu zitatolewa kwa mfumo wa Tiketi Mtandao na kuwa Mamlaka inaendelea kufanya kaguzi na kutoa elimu kabla ya kuanza kutoa adhabu.

 

 “Tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha wananchi wanaelewa, na wale ambao bado hawajaingia kwenye mfumo wanaingia, kwa kuanzia tunakutana kila mwezi ili kuendelea kutatua changamoto na kuhakikisha mabadiliko ya mfumo huu yanazoeleka.” Alisema.

 

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Swalehe Byarugaba alisema “Lengo la mfumo huu ni kuhakikisha msafirishaji anakua na nyaraka moja ambayo itasimama kama risiti na wakati huohuo kama tiketi ya abiria, nashkuru uongozi wa TABOA na wadau wengine, tumekubaliana tiketi zote zitolewe kwa njia ya mtandao.”

 

Naye Mwenyekiti wa TABOA, Abdallah Kiongozi amesema kuwa kikao hicho ni mwendelezo wa kuboresha mfumo wa tiketi mtandao na kuwa mfumo huu ni mzuri kwa kuwa unawasaidia wamiliki, Mamlaka za Serikali na Abiria, huku akiwaasa wananchi na wasafirishaji kuunga mkono juhudi za Serikali.

 

Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA Johansen Kahatano amesema kwa mfumo wa Tiketi Mtandao kwa sasa umeboreshwa baada ya changamoto mbalimbali zilizokuwepo kupatiwa ufumbuzi kwa kushirikisha Serikali na wamiliki wa mabasi.

 

Aliongeza kuwa, LATRA imewafikia wamiliki wa mabasi wa kanda zote Tanzania Bara katika kazi ya kutoa elimu na kupokea maoni iliyofanyika kwa miezi mitatu ya Aprili, Mei na Juni 2022.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo