Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeongeza muda wa siku 90 kwa madereva wa vyombo vya moto kibiashara kujitokeza kwa hiari ili kusajiliwa na kufanyiwa ithibati.
Akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara amesema ongezeko la siku hizo ni kutokana na sababu mbalimbali zilizowafanya baadhi ya madereva kushindwa kujisajili kwa wakati uliopangwa hapo awali.
"Tumegundua sababu mbalimbali zilizofanya madereva washindwe kujitokeza kujisajili, kama vile uhitaji wa dereva kufanyiwa vipimo vya afya kama moja ya vipengele muhimu, na madereva kutopita katika shule rasmi za kujifunzia udereva, hivyo kwa kuzingatia hilo tumeongeza muda wa kuwasajili madereva kwa miezi mitatu (3) zaidi mpaka Julai 31 mwaka huu," amesema Bw. Kahatano.
Akiongelea faida za madereva kusajiliwa, Bw. Kahatano amesema usajili wa madereva utafanya fani ya udereva kutambulika kama taaluma rasmi kama zilivyo taaluma nyingine, pia kuwaongezea madereva wigo wa ajira katika Jumuiya mbalimbali ambazo Tanzania ni mwanachama.
"Usajili wa madereva utafanya fani ya udereva kufahamika rasmi kama taaluma nyingine, pia nchi yetu ipo kwenye Jumuiya mbalimbali kama vile SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa usajili huu madereva wanakuwa wamekidhi kupata uhalali wa kupata ajra katika nchi yoyote ambayo nchi yetu ni mwanachama, pia tunaweza kutambua katika muda fulani ni dereva gani anaendesha chombo kupitia kifaa cha i-button," ameongeza Bw. Kahatano.
Aidha Bw. kahatano amesema kuwa, kuanzia Mei 1, 2023 magari yanaweza kusafirisha abiria kuanzia saa 9 na saa 10 alfajiri hivyo kwa wasafirishaji wenye uhitaji wanaweza kuomba ratiba ya njia mbalimbali ili kuanza safari hizo.
"Tumefanya majaribio kwenye njia baadhi ili kuangalia namna usafirishaji utakavyokuwa na namna ya kudhibiti kwa kusafirisha abiria kuanzia saa 11 alfajiri, baada ya kujiridhisha na majaribiio hayo kuanzia tarehe 1 Mei, 2023 Mamlaka itaanza kutoa ratiba za kuanza safari saa 9.00 na 10.00 usiku kwa watoa huduma wenye kuhitaji, hata hivyo, madereva wa magari haya watapaswa kuwa wamesajiliwa na wanatumia kifaa maalum cha kumtambua dereva anayeendesha gari (i-button)," amesema Bw. Kahatano.
Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani SACP Ramadhani Ng'anzi amewahimiza wamiliki wa shule za madereva kufuata vigezo na masharti yaliyowekwa ili kuzalisha madereva walio bora.
"Tumefungia shule nyingi za udereva kutokana na kutokidhi vigezo mbalimbali, hivyo niwahimize kufuata masharti yaliyowekwa ili waweze kufunguliwa, shule hizi zikifuata vigezo vilivyowekwa nina uhakika hata madereva watakaozalishwa watakuwa bora," amesema SACP Ng'anzi.
Mnamo Februari 22, 2023, Mhe. Mha. Hamad Masauni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alitangaza kuwa madereva wote wa vyombo vya moto kibiashara wahakikishe wamesajiliwa LATRA kabla ya tarehe 30 Aprili, 2023, madereva mbalimbali wameweza kujitokeza ili kufanyiwa usajili ambapo mpaka sasa takribani madereva 3334 wamejitokeza na kufanyiwa usajili.