Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAPONGEZWA KWA KUANDAA MKUTANO NA WADAU WA TEKSI MTANDAO
Imewekwa: 11 Oct, 2022
LATRA YAPONGEZWA KWA KUANDAA MKUTANO NA WADAU WA TEKSI MTANDAO

Na. Mambwana Jumbe

Mkuu wa Wilaya Ilala Mhe. Ng'wilabuzu Ndatwa Ludigija ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kutekeleza dhana ya ushirikishaji kama moja ya msingi wa utawala bora kwa kuandaa mkutano wa wadau wenye lengo la kupokea maoni kuhusu marejeo ya viwango vya nauli ya teksi mtandao

Mhe. Ludigija amesema hayo Oktoba 11, katika ukumbi wa Arnatoglou alipofungua Mkutano wa Wadau kuhusu marejeo ya viwango vya nauli za Teksi Mtandao nchini kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla

Aidha, Mhe. Ludigija amesema “moja ya misingi ya utawala bora ni ushirikishwaji, nasi kama wadau kwa upande wa Serikali tumefurahi kushuhudia ushiriki wenu wadau katika Mkutano huu muhimu wa kutoa maoni yenu ili kuipa LATRA taarifa zitakazoisaidia kufanya maamuzi.”

Ameongeza kuwa, Usafiri wa magari ya kukodi ni muhimu katika kuongeza wigo wa huduma za usafiri kwa abiria hususan mijini, ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa wakati na kuboresha maisha ya Watanzania.

Vilevile amewapongeza wabunifu na wawekezaji wote ambao wametengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayowezesha kusimamia huduma za usafiri wa teksi mtandao lakini pia ameitaka LATRA kuongeza usimamizi wa utendaji wa mifumo hiyo kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo, kwa kujali maslahi mapana ya watumia huduma, wawekezaji na wananchi wote kwa jumla.

“Kwa kuwa jukumu tunalofanya leo ni kupokea mapendekezo, kuyajadili na kutoa maoni, nawasihi kila mmoja wetu, kwa kuzingatia wajibu wake, kutoa maoni yake kwa uhuru na kwa lugha yenye staha. Natoa rai kwenu wadau kuitumia vizuri nafasi hii, ili kuwawezesha wataalamu wetu kufanya kazi yao kwa ufanisi”, ameeleza Mhe. Ludigija.

Naye Mkurugenzi Mkuu LATRA CPA Habibu Suluo amesema Kwa mujibu wa Kifungu cha 19 (3) cha Sheria Sura 413, baada ya kuzingatia maoni ya wadau, Mamlaka ilitangaza Nauli Elekezi za teksi mtandao kwa Tangazo Na. LATRA/01/2022 la tarehe 14/3/2022 ambalo lilitolewa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 8/4/2022 kwa Tangazo Na. 1369 ambalo liliainisha viwango vya nauli ya teksi mtandao.

Aidha, amesema kuwa,  wakati wa utekelezaji wa nauli za teksi mtandao, Mamlaka kwa nyakati tofauti, ilipokea malalamiko kutoka kwa wadau hawa (Bolt na Uber) lakini pia kutoka kwa madereva wa teksi mtandao kupitia chama chao – Tanzania Online Drivers Association (TODA) na hivyo Mkutano huo umeandaliwa ili kupokea maoni kuhusu viwango vya nauli vilivyopo ili kutatua changamoto zao.

CPA Suluo ameongeza kuwa, baada ya kukamilisha zoezi la kupokea maoni ya wadau, Menejimenti ya LATRA itafanya tathmini na kuwasilisha mapendekezo kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya LATRA kwa uamuzi na mapendekezo ambayo yatawasilishwa kwa Mamlaka za Serikali (Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali). Baada ya idhini ya Mamlaka za Serikali, nauli zitatangazwa kwenye Gazeti la Serikali, na zitaanza kutumika siku 14 baada ya kutangazwa kwa mujibu wa Kanuni.

Mkutano huo ulioandaliwa na LATRA, umefanyika katika ukumbi wa Arnatoglou uliopo mnazi mmoja Dar es Salaam, umehusisha wadau mbalimbali kama vile Makampuni ya Teksi Mtandao (Bolt, Uber,Little Ride, Paisha, InDrive, nk), Madereva wa Teksi Mtandao, Wamiliki wa Magari ya Teksi Mtandao, Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) na wadau wengine.

Pakua hotuba ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam 

Pakua hotuba ya Mkurugenzi Mkuu

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo