
DCP Johansen Kahatano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), amesema kuwa Mamlaka imetanua wigo wa upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kwa kuanzisha njia mpya za usafiri wa umma katika maeneo ya miji na kuzifanyia mapitio njia za zamani kwa kuzirefusha au kuzifanya za mzunguko, pia imeanzisha njia mpya hususan zinazounganisha Jiji la Dodoma na maeneo mengine ya nchi.
DCP Kahatano amebainisha hayo alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za udhibiti usafiri ardhini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika kikao kilichofanyika Januari 15, 2025 Ukumbi wa Mikutano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameongeza kuwa, Mamlaka imeendelea kutekeleza shughuli za kiudhibiti kwa ufanisi katika Usafiri wa Barabara, Usafiri wa Reli pamoja na Usafiri wa Waya.
Alizungumzia jukumu la utoaji wa Leseni na usimamizi wa masharti yake kwa upande wa usafiri wa barabara, amesema huduma za Usafiri wa barabara zimeimarika ikiwemo kuongezeka kwa maombi ya leseni za usafirishaji katika njia mpya na zilizokuwepo ambapo idadi ya leseni za usafirishaji iliongezeka kwa jumla ya asilimia 42 kutoka leseni 230,253 katika mwaka wa Fedha 2020/21 hadi kufikia leseni 326,576 katika Mwaka wa Fedha 2023/24.
“Sekta imeonesha kuimarika kutoka katika athari za UVIKO-19 zilizojitokeza mwaka 2020/21 na 2021/22 ambazo zilisababisha huduma zinazoombewa leseni kuongezeka kwa kiwango kidogo katika miaka hiyo. Athari zilionekana katika Sekta ya utalii na biashara ambazo ni miongoni mwa wadau wakubwa katika soko la usafiri na usafirishaji. Kufikia mwaka 2022/2023, leseni za huduma ziliongezeka kwa asilimia 18 na mwaka 2023/2024 zikaongezeka kwa asilimia 15 kulinganisha na asilimia 4 kwa mwaka 2021/2022, ambapo katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2020/21 hadi 2023/24 jumla ya leseni 1,080,940 za usafirishaji kwa njia ya barabara zilitolewa,” ameeleza DCP Kahatano.
Vilevile amesema, Mamlaka imetekeleza maelekezo ya Serikali ya kuanzisha na kusimamia huduma za mabasi kwa saa 24, “Utekelezaji huu ulianza tarehe 1 Oktoba, 2023 kwa kutoa masharti mahsusi kwa watoa huduma waliomba ratiba za kufanya safari za usiku. LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tumeendelea kusimamia huduma hizi ambazo zimeonekana kuwa ni chaguo la wananchi wengi lenye tija ya matumizi ya muda wa mchana kwa shughuli za uzalishaji, gharama za kulala njiani na utulivu wa safari”.
Akizungumzia pikipiki za magurudumu mawili na matatu amesema,“Tumeanza kutoa elimu ya vyama vya ushirika na kuhamasisha vijana waendesha pikipiki kujiunga katika vyama vya ushirika na kupewa uwakala wa LATRA. Zoezi hili linaenda vizuri na tayari mkoa wa Kilimanjaro una chama (KIBABOT) na unafanya vizuri”.
DCP Kahatano alisema LATRA imeendelea kudhibiti huduma za usafiri wa reli ambapo katika reli ya kisasa (SGR) Mamlaka iliidhinisha nauli za abiria kwa huduma za kawaida mwezi Juni 2024 ambapo kati ya Dar-es-Salaam na Dodoma ni Shilingi 31,000 kwa daraja la kawaida na Shilingi 50,000 kwa huduma ya haraka katika daraja la kawaida.
Kwa upande wa usafiri wa waya, ameishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kuandaa rasimu ya Kanuni za udhibiti wa usafiri huo ambazo zimeshawasilishwa kwa wadau kwa ajili ya kupokea maoni yao. Usafiri wa waya hutumika katika maeneo yenye milima na vivutio vya utalii kama Arusha na Kilimanjaro. Hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii nchini ambapo kwa sasa idadi ya watalii imeongezeka.
Naye Mhe. Moshi Selemani Kakoso (Mb) ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu alipongeza jitihada zilizofanyika na ameitaka Mamlaka kufuata na kutekeleza maoni ya wajumbe yaliyotolewa katika kikao hicho ili kuendelea kuboresha huduma za sekta ya usafiri ardhini nchini.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).