Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YAWAKABIDHI POLISI VIPIMA ULEVI 3,050 ILI KUIMARISHA USALAMA BARABARANI
Imewekwa: 07 Jan, 2025
LATRA YAWAKABIDHI POLISI VIPIMA ULEVI 3,050 ILI KUIMARISHA USALAMA BARABARANI

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura amesema Jeshi la Polisi limeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ajali za barabarani ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyokuwa akiyatoa mara kwa mara ya kuhakikisha ajali za barabarani zinadhibitiwa ipasavyo.

IGP Wambura ameyasema hayo wakati akipokea vifaa 3,050 kati ya 10,000 vya kupima ulevi kwa madereva vilivyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambapo CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA alikabidhi vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Polisi Jijini Dodoma Januari 6, 2024.

IGP Wambura alisema kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani watakuwa wakali kwa madereva wazembe ambao wamekuwa wakisababisha ajali za barabarani ambapo pia wataendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kuwa watanzania wanakuwa salama.

“Tumeweza kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali na sasa nguvu pia tunazielekeza kwenye usalama barabarani kwa kuwa takwimu za ajali bado zipo juu hivyo ni lazima tuwe wakali sana ili kuona sheria za usalama barabarani zinafuatwa ili kuokoa maisha ya Watanzania” Alisema IGP Wambura.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) CPA Habibu Suluo amesema, utendaji kazi wa LATRA unahitaji sana ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kusimamia Sheria za Usalama Barabarani na hivyo vipima ulevi hivyo vitasaidia Kikosi cha Usalama Barabarani katika kudhibiti ajali za barabarani zinazosababishwa na madereva walevi na wazembe pindi wanapokuwa barabarani na kuendesha pasipo kuzingatia sheria.

CPA Suluo alisema uwepo wa vifaa hivyo utasaidia kupima madereva mara kwa mara wawapo barabarani jambo ambalo litasaidia kufanya barabara zetu kuwa salama.

Aidha alisema LATRA itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutumia mifumo katika kufanya ukaguzi wa magari ambapo kwa sasa wanaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali.

Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo ilihudhuriwa na Makamishna wa Polisi, Manaibu Kamishna wa Polisi, baadhi ya Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi na Maofisa kutoka LATRA

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo