Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA 15 WASITISHIWA LESENI
Imewekwa: 12 Apr, 2023
MADEREVA 15 WASITISHIWA LESENI

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesitisha leseni za madereva 15 wa mabasi ya masafa marefu waliohusika kuharibu Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) ili mabasi yao yakimbie pasipo kuonekana kwa kipindi cha mwezi Machi, 2023.

Hayo yamezungumzwa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani– SACP Ramadhani Ng’anzi kwenye kikao na waandishi wa habari kilichofanyika Aprili 11, 2023 katika ofisi za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Dar es Salaam.

SACP Ng’anzi amesema kuwa suala la udhibiti usalama barabarani ni endelevu na Jeshi la Polisi halitovumilia kuona maisha ya watanzania yanawekwa rehani na madereva wasiofuata Sheria.

“Tulifanya ukaguzi wa Mfumo wa VTS na tuligundua mfumo huo umechezewa na sisi tukachukua hatua ya kuwafungia madereva na baadhi yao kuwafutia kabisa leseni zao. Tutaendelea kudhibiti mienendo ya madereva na niwasihi madereva wote kufuata Sheria za Usalama Barabani ikiwemo kuendesha basi kwa mwendo wa Kilometa 80 kwa saa,” amesisitiza SACP Ng’anzi.

Naye Mkurugenzi Mkuu LATRA-CPA Habibu Suluo amewakumbusha wamiliki na madereva wote wa vyombo vya moto kibiashara kuhakikisha wamekamilisha usajili wa madereva kupitia https://rrims.latra.go.tz/ ifikapo Aprili 30, 2023 kama ilivyotangazwa hapo awali.

“Kwa mujibu wa masharti ya leseni za kutoa huduma ya usafirishaji, wamiliki wote wa vyombo vya usafiri kibiashara wanatakiwa kuwa na madereva ambao wamesajiliwa na kuthibitishwa. Ili kusajiliwa, dereva anatakiwa kuwa na leseni hai ya udereva, cheti cha mafunzo ya udereva na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA),” amefafanua CPA Suluo. 

Pakua orodha ya madereva waliofungiwa 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo