Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MADEREVA BAJAJI NA BODABODA WAASWA KUJIWEKEA AKIBA ILI KUJIKWAMUA KIUCHUMI
Imewekwa: 04 May, 2023
MADEREVA BAJAJI NA BODABODA WAASWA KUJIWEKEA AKIBA ILI KUJIKWAMUA KIUCHUMI

Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Bw, Johansen Kahatano amewasihi wamiliki na madereva wa pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na matatu (bajaji) mkoani Kilimanjaro kuanza tabia ya kujiwekea akiba ya fedha ili kuweza kujikimu kiuchumi.

Bw. Kahatano amesema hayo kwenye kikao cha kupokea taarifa ya Kamati ya Uratibu wa Mchakato wa Uanzishwaji wa Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa wamiliki na madereva wa pikipiki za magurudumu wawili (bodaboda) na matatu (bajaji) kilichofanyika Mei 4, 2023 katika ukumbi wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Manispaa ya Moshi mjini Mkoani Kilimanjaro.

Vilevile, Bw. Kahatano amesema, kazi ya kuendesha bajaji na bodaboda ni kama kazi nyingine, hivyo amewakumbusha madereva na wamiliki hao kuheshimu na kuonesha weledi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao,"Nawasihi kuwa mabalozi wazuri kwa madereva wenzenu kote nchini kwa kufuata Sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinapunguza nguvu kazi ya Taifa."

Naye Bw. Patrick Boisafi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango wa maafisa wasafirishaji nchini na imeweka ahadi ya kuwasaidia vijana kupitia vyama vya ushirika

“Nawapongeza sana LATRA, Jeshi la Polisi na kamati nzima kwa kutekeleza maono ya Serikali yetu na niwasihi sana walengwa kuwa muendelee kuwa na umoja na mshikamano ili kufikia malengo mliyojiwekea. Mtafundishwa jinsi ya kuweka akiba, mkazingatie na muwe na utaratibu wa kuweka akiba kidogokidogo,” amesisitiza Bw. Boisafi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Bw. Mohammed Nkya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Mchakato wa Uanzishwaji SACCOS hiyo amesema wataendelea kushirikiana na wamiliki na madereva wa bajaji na bodaboda Mkoani hapo na kuhakikisha wanajikwamua kiuchumi.

Akizungumzia faida za SACCOS kwa madereva na wamiliki wa bodaboda na bajaji, Afisa Mfawidhi wa LATRA mkoa wa Kilimanjaro Bw. Paul Nyello amesema itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi, itakuwa rahisi kwa Mamlaka kuwaratibu wakiwa katika majukumu yao, itawasaidia kukua kiuchumi na kuweza kusaidiana wao wenyewe na kikubwa zaidi itangeza heshima ya kazi wanayoifanya.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo