Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAGOMBANA: MAONI YENU NI MUHIMU ILI KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI NCHINI
Imewekwa: 05 Jun, 2024
MAGOMBANA: MAONI YENU NI MUHIMU ILI KUBORESHA HUDUMA ZA USAFIRI ARDHINI NCHINI

Wadau wa usafiri ardhini wamesisitizwa kutoa maoni yao kuhusu Sheria ya Leseni za Usafirishaji Sura ya 317, Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura 413 na Kanuni zake, ili kuboresha huduma za usafiri ardhini nchini.

Hayo yameelezwa na Bw. Andrew Magombana, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa Njia ya Barabara kutoka Wizara ya Uchukuzi aliyemuwakilisha Prof. Godius Kahyarara, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, katika kikao cha wadau cha kupokea maoni kuhusu maboresho ya Sheria ya Leseni za Usafirishaji Sura ya 317, Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura 413 na Kanuni zake, kilichofanyika Juni 05, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Arnaoutouglou, Jijini Dar es Salaam.

Bw. Magombana amezitaja kanuni hizo kuwa ni Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Huduma ya Kukodi) za Mwaka 2020, Kanuni za Leseni (Huduma za Usafiri wa Umma) za Mwaka 2020, Kanuni za Leseni (Vyombo vya kubeba mizigo) za Mwaka 2020, Kanuni za Utaratibu wa Kushughulikia Malalamiko za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za Mwaka 2024, pamoja na Kanuni za Vigezo na Masharti ya Kutoa Huduma zinazodhibitiwa za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2024.

“Kwa maoni yenu, tunaweza kupata maboresho ya Sheria na Kanuni ambayo  yatasaidia shughuli za Mamlaka ya  Udhibiti  Usafiri Ardhini (LATRA)  na kuleta matokeo chanya kwa nchi yetu ikiwa ni pamoja na  kuwa na huduma za usafiri zilizo salama, za uhakika na rafiki kwa mazingira,” amesisitiza Bw. Magombana.

Naye CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amesema kuwa, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza suala la ushirikishaji wa wadau ambalo limekuwa likitekelezwa kwa vitendo na Wizara ya Uchukuzi na LATRA ndio maana mkutano umeandaliwa na wadau wameshirikishwa na kuwa huru kutoa maoni yao ambayo yatafanyiwa kazi.

Vilevile ameeleza kuwa, LATRA inashirikiana vizuri na wadau wake, pia Wizara ya Uchukuzi na Mamlaka wanataka kuwa na Sheria rafiki inayowajali na itakayosaidia kukuza mitaji ya wasafirishaji ili waweze kutekeleza shughuli zao za kuwahudumia wananchi kupitia usafirishaji, “tunachokifanya leo, si mwisho na tutakuwa na nafasi ya kukutana na kufanya maboresho ya Sheria na Kanuni zetu mara kwa mara ili kuwa na sekta ya usafirishaji yenye tija na manufaa kwa wananchi, wasafirishaji na Serikali kwa jumla.”

Pia, CPA Suluo amesema wadau hao na wale ambao hawakuweza kufika katika mkutano huo, waendelee kutuma maoni yao kwa maandishi kupitia baruapepe ya group.maoni@latra.go.tz mpaka tarehe 12 Juni, 2024.

Naye Bi. Mwadawa Sultan, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria kutoka LATRA amesema sababu za kufanya maboresho ya Sheria ambazo ni kufuta baadhi ya majukumu ambayo hayatekelezeki kwa Mamlaka kwa kuwa yanaratibiwa na Taasisi nyingine za Serikali, kutoa tafsiri ya maneno mbalimbali ambayo yalikuwa hayana tafsiri mahsusi, kutambulisha Mawakala wa Mamlaka katika Sheria zote mbili na Kanuni zote chini ya Sheria za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini na kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya vifungu mfano kufafanua ni mazingira gani yanaweza kupelekea mgongano wa maslahi,

Pia, Bi. Mwadawa amesema sababu nyingine ni kufuta utaratibu wa zamani wa utoaji wa leseni uliotolewa chini ya Sheria ya leseni (Transport licencing Act Cap 317) ambao ulikuwa chini ya mamlaka za Uteuzi (appointing Authorities) na kuweka wa sasa ambao upo chini ya Mamlaka ya leseni (Licencing authority) ambayo ni LATRA, kuendana na uhalisia wa mazingira yalivyo sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia na gharama za uendeshaji kwa ujumla pamoja na  kuweka bayana muda kukata rufaa kwa ambaye hajaridhika na maamuzi ya Bodi kwenda  katika Baraza la Ushindani ndani ya siku 14, ambapo kwa sasa Sheria ya LATRA  haijataja muda.

Vilevile Bi. Mwadawa ameainisha sababu za kufanya maboresho ya Kanuni kuwa ni viwango vilivyopo ni vya muda mrefu haviendani na hali halisi ya mabadiliko ya uchumi na biashara, kutenganisha kati ya huduma za mabasi ya abiria kwa umma na huduma za vyombo vya kukodi, kutenganisha adhabu kwa vyombo vya usafiri kulingana na uwezo wa chombo husika mfano malori makubwa na vyombo vidogo vya kubeba mizigo kama vile pikipiki za magurudumu matatu (guta)

Ameongeza kuwa, sababu nyingine ni kutambua Kanuni zilizotengenezwa kwa ajili ya Ufifilishaji wa Makosa na adhabu ili zitumike ipasavyo na kupendekeza kufutwa kwa kanuni zinazobainisha ufifilishaji wa makosa kwenye Kanuni hizi, Kwa Kanuni za mwaka 2024, sababu kubwa ni utekelezaji wa maoni ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria ndogo.

Wadau mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wameipongeza Wizara ya Uchukuzi na LATRA kwa jitihada za dhati za kuboresha sekta ya usafiri ardhini nchini na wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwa na sekta ya usafiri iliyo bora.

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo