Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MAUPIDA YATUNUKIWA CHETI CHA UWAKALA WA LATRA
Imewekwa: 14 Aug, 2025
MAUPIDA YATUNUKIWA CHETI CHA UWAKALA WA LATRA

Mhe. Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala ametunuku Cheti cha Uwakala wa kutoa leseni za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri ardhini (LATRA) kwa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Maafisa Usafirishaji wa Pikipiki Dar es Salaam (MAUPIDA SACCOS) Agosti 13, 2025 kwenye hafla iliyofanyika ukumbi wa Golden Jubilee, Dar es Salaam.

Akikabidhi cheti hicho kwa niaba ya Mhe. Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Mpogolo amewapongeza MAUPIDA SACCOS LTD kwa kuwa mawakala rasmi wa LATRA huku akiwasihi kuhamasishana kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ikiwemo kuhakikisha kila chombo kinachotoa huduma ya usafirishaji kinakuwa na leseni.

“Muhimizane ninyi kwa ninyi kufuata alama za barabarani, kuendesha kwa mwendo unaokubalika kwa mujibu wa Sheria, epukeni kufanya vitendo vinavyohatarisha maisha yenu mkiwa katika kazi zenu na kikubwa zaidi mkumbuke kuwa ninyi ni nguvukazi ya Taifa lakini pia mnategemewa na familia zenu, hivyo usalama unatakiwa kuwa kipaumbele chenu,” amesema Mhe. Mpogolo.

Vilevile Mhe. Mpogolo amesema cheti cha uwakala wa LATRA walichopatiwa ni alama ya uaminifu, uadilifu na fursa, hivyo wanapaswa kukitumia vizuri ili kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi ya maendeleo itakayowawezesha kutimiza malengo yao kupitia uwakala waliopata kwa kutoa huduma bora na salama za usafiri kwa wananchi.

Aidha Mhe. Mpogolo amebainisha kuwa, yeye kama mlezi atashirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha ushirika huo unakuwa kinara na wa mfano nchini, “Tutaendelea kushirikiana kwa ukaribu pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha mnafikia malengo mliyojiwekea na pia tutahakikisha shughuli za usafirishaji zinafanyika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Miongozo iliyopo. Tunataka kuona Pikipiki za magurudumu mawili, matatu, daladala, na watoa huduma wengine wa usafiri ardhini wakifanya kazi katika mazingira yenye mpangilio mzuri, salama na tija kwa jamii na Taifa kwa jumla.”

Naye DCP Johansen Kahatano, Mkurugenzi Udhibiti Usafiri wa Barabara LATRA aliyemuwakilisha CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema kuwa, Mamlaka inafanya jitihada ya kuwaunganisha pamoja maafisa usafirishaji kwa kuwapatia elimu na kuwashawishi kujiunga na kuanzisha vyama vya ushirika ambavyo vitawasaidia kuweka akiba na kuwaongezea kipato.

“LATRA inalenga kuondoka kwenye utaratibu wa kudhibiti mtu mmoja mmoja na kwenda kwenye mfumo wa udhibiti kupitia vyama vya ushirika au kampuni ambapo wasafirishaji watainuana kiuchumi, kusimamiana wenyewe na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao wakizingatia masharti ya leseni za usafirishaji walizonazo bila kushurutishwa,” ameeleza DCP Kahatano.

Kwa upande wake Bw. Atanas Kitime, Mwenyekiti wa Bodi ya MAUPIDA SACCOSS LTD amemshukuru Mhe. Mpogolo kwa kuwa nao bega kwa bega na kuwawezesha kufanikisha uazishwaji wa chama hicho ambao unaenda kubadili maisha yao na pia ameishukuru LATRA kwa kuweka asilimia 20 ya gawio watakalolipata kutokana na leseni watakazozikata.

“Tuna matumaini makubwa kuwa hali zetu za maisha zinaenda kuboreka kupitia ushirika wetu ukizingatia tunaenda kunufaika na 20% ya mapato tutakayokusanya huku tukichangia pato la Taifa. Pia, tutahakikisha ukataji wa leseni za usafirishaji unaongezeka na tutatekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa Sheria,” amesema Bw. Kitime.

Bw. Said Kagoma, Mwenyekiti wa Shirikisho la MAUPIDA amewataka waendesha bodaboda kuzingatia Sheria za usalama barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu (helmet) kubeba abiria kwa usahihi na kuendesha kwa uangalifu ili kuepusha ajali ambazo zinaepukika.

MAUPIDA SACCOS LTD wamepatiwa cheti cha uwakala ambacho kitawaruhusu kutoa aina sita za leseni za vyombo vya moto vya kukodi ambazo ni leseni za Pikipiki za Magurudumu Mawili, Leseni za Pikipiki za Magurudumu Matatu, Leseni za Taksi za kawaida, Leseni za Taksi Mtandao (Ride Hailing), Leseni za Magari Maalumu ya Kukodi (Special Hire) pamoja na Leseni za Kuitisha Mtandaoni Usafiri wa Kuchangia (Ride Sharing).

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo