Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

NW KIHENZILE AKOSHWA NA MFUMO WA PIS
Imewekwa: 25 Oct, 2024
NW KIHENZILE AKOSHWA NA MFUMO WA PIS

Mhe. David Mwakiposa Kihenzile (Mb), Naibu Waziri - Uchukuzi amekoshwa na jinsi Mfumo wa Taarifa kwa Abiria (PIS) unaopatikana kwa anwani www.pis.latra.go.tz unavyowawezesha abiria wa mabasi ya masafa marefu kupata taarifa za mabasi yanayotarajiwa kuwasili katika stendi iliyo karibu yao pamoja na kufahamu mwendokasi wa basi husika wakiwa safarini.

Mhe. Kihenzile ametoa pongezi hizo Oktoba 25, 2024, alipotembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika maonesho ambayo ni sehemu ya Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Kutathmini Utendaji kazi wa Sekta ya Uchukuzi yaliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Akiueleze Mfumo huo, CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu LATRA amesema PIS inaokoa muda wa mtu kumsubiri mgeni wake anayetarajia kuwasili na basi kwa kuwa kupitia mfumo ataona muda na mahali basi lilipo na hivyo kufanya makadirio ya kutoka alipo na kwenda stendi kumpokea mgeni wake.

“Nitumie furasa hii kuwaasa wananchi kutumia mfumo wa PIS na watoe taarifa za mwendokasi kwa kutupigia kwa namba zetu bila malipo 0800110019 au 0800110020 nasi tutachukua hatua stahiki,” amesema.

Wakati huohuo CPA Suluo amemweleza Mhe. Kihenzile kuwa, LATRA inatumia mfumo wa e-mrejesho kupata maoni, mapendekezo, pongezi na malalamiko kutoka kwa wananchi na umesaidia kuboresha huduma za Mamlaka.

Vilevile ameeleza kuwa, LATRA imeendelea kudhibiti usafiri wa reli na kwa sasa huduma za treni ya kisasa zinaendelea ambapo treni ya EMU maarufu kama treni ya mcongoko nayo inatarajiwa kuanza safari zake hivi karibuni.

Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Sekta ya Uchukuzi umefanyika Oktoba 23 hadi 25, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo