Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

PROF. AME AWASIHI WASAFIRISHAJI KUAJIRI MADEREVA WENYE SIFA NA TABIA NJEMA
Imewekwa: 01 Aug, 2025
PROF. AME AWASIHI WASAFIRISHAJI KUAJIRI MADEREVA WENYE SIFA NA TABIA NJEMA

Prof. Ahmed Mohamed Ame, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) amewasihi wasafirishaji nchini kuajiri madereva wenye sifa na tabia njema ili kusaidia kupunguza ajali barabarani.

Prof. Ame amesema hayo kwenye ziara ya Bodi ya Wakurugenzi LATRA kwa Kampuni ya Superdoll, Dar es Salaam Agosti 01, 2025,

Prof. Ame ameeleza kuwa, ni muhimu wasafirishaji wengine kujifunza kutoka kampuni ya Superdoll kuhusu namna wanavyowapata madereva wao kwa kuzingatia tabia (character), uwezo (competency) na namna dereva anaweza kufanya kazi na wengine (chemistry) ili kupata matokeo wanayotaka. 

“Watoa huduma wengine nao kuna haja ya kujifunza kutoka Superdoll kwa kuwa wanafanya mambo makubwa ya usalama barabarani na wakiweza kutekeleza hata asilimia 20 tu ya wanayotekeleza kampuni hii itasaidia sana kupunguza ajali barabarani,” amsema Prof. Ame.

Vilevile amesema, Superdoll ni kampuni iliyoweka kipaumbele na kuwekeza sana kwenye suala la usalama barabarani, hivyo wamejifunza mbinu mbalimbali ambazo watazitumia katika kuboresha na kujenga mifumo ya kiudhibiti.

“Tukitazama mfumo wao wa kufuatiia magari jinsi unavyoenda na muda, unamuona dereva na vitendo vyake akiwa safarini ambapo si tu mfumo unapeleka taarifa kwa wataalam wao lakini pia unamuarifu dereva kuhusu vitendo hivyo vinavyohatarisha usalama anavyofanya akiwa barabarani. Hii inasaidia sana kiusalama kwa kuwa dereva anajirekebisha papo hapo baada ya kukumbushwa na mfumo unaomuongelesha kwa sauti,” amesema Prof. Ame.

Akizungumzia suala la kudhibiti uchovu wa madereva wawapo safarini, Prof. Ame amesema Superdoll wanatumia mfumo kusimamia uchovu wa dereva na kwa upande wa LATRA kwa sasa wanaandaa Kanuni na kupitia ushirikiano uliopo, Kampuni hiyo nayo itatakiwa kutoa maoni yao ili kupata Kanuni zitakazotatua changamoto hiyo.

Katika hatua nyingine, Prof. Ame amefafanua sababu ya Bodi ya LATRA kufanya ziara kwenye Kampuni hiyo, “Taarifa zetu zinaonesha kwamba Superdoll ni miongoni mwa wadau wetu wanaofanya vizuri sana kwa hiyo tukawa na ari kubwa ya kuja kumtembelea kwa lengo la kujifunza. Dira yao inaonesha wanataka kuwa wasafirishaji bora Afrika Mashariki na Kati lakini ukweli ni kwamba ni watoa huduma za usafirishaji wakubwa Afrika, hakuna wa kupinga, kampuni hii imetoa huduma kilomita milioni 45 bila kupata ajali”.

Naye Bw. Ibrahim Juma, Meneja Mkuu Kampuni ya Superdoll amewasihi wasafirishaji kuwajengea uwezo madereva wao kwa kuwaongezea ujuzi kupitia mafunzo ili kuongeza tija na thamani yao katika kazi wanayoifanya na hatimaye kuwa na sekta ya usafirishaji yenye usalama.

Pia, ameishukuru Bodi ya LATRA na ameiomba kuendeleza ushirikiano uliopo ili kwa pamoja wafikie lengo la kuwa na sekta ya usafirishaji yenye tija na manufaa kwa Serikali, Wasafirishaji na Wananchi kwa jumla.

LATRA inautaratibu wa kuwatembelea wadau wake ili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kudhibiti sekta ya usafiri ardhini nchini kwa kuwa maendeleo ya sekta hii yanahitaji mchango wa kila mdau.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo